Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameipongeza wakala wa ujenzi wa barabara za vijijini TARURA kwa ubunifu wanaoutumia katika ujenzi wa madaraja ya mawe yanayowaunganisha wananchi katika maeneo ya vijijini na barabara muhimu katika shughuli zao za biashara na huduma za kijamii na kiutawala.
Waziri Mchengerwa amesema ubunifu wanaoutumia TARURA ni jambo linalohitaji kupongezwa kwa namna wanavyo ishirikisha jamii husika katika ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja na maeneo korofi ambayo yamekuwa kero kwa wnanachi kwa muda mrefu.
Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Kigoma, alipotembelea daraja la mawe la Bweru liliko kijiji cha Mgalaganza halmashauri ya Kigoma Vijijini , linalo ziunganisha kata za Bitale na kata ya Kagongo lilojengwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania kupitia wakala wa barabara za vijijini TARURA na ubalozi wa Uberigiji likigharimu milioni 101, huku mchango wa wananchi katika ujenzi huo ukiwa ni nguvu kazi ya kusogeza mawe na vifaa wakati wa ujenzi mchango huo ukithaminishwa kuwa shilingi milioni tatu kwa ujumla wake.
“TARURA nawapongeza kwa kuendelea kuwa wabunifu na kuwezesha mawasiliano baina ya kijiji na kijiji, kata na kata na halmashauri na halmashauri, kwakweli mnafanya kazi nzuri, ujenzi wa daraja hili ni hatua tosha inayowafanya mstahili kupongezwa” alisema Waziri Mchengerwa.
“ Tumeelezwa na mtaalam kuwa kama daraja hili lenye urefu wa mita 27, lingejengwa kwa mfumo wa kawaida basi lingegharimu zaidi ya shilingi milioni 600, lakini kwa ujenzi wa mfumo huu au teknolojia hii ya mawe na ushirikishwaji wa wananchi limegharimu shilingi milioni 101, hili ni jambo la kupongeza na huu ndiyo ubunifu tunaousisitiza” aliongeza waziri Mchengerwa.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Kigoma vijini Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma Mhe. Joseph Nyambwe amesema wenyeji wanautafasiri ujenzi wa daraja hilo kama ukombozi wao katika hali duni ya kimaisha kwani sasa wataweza kusafiri kwa urahisi na kusafirisha mazao yao ya chakula na biashara kwa uhakika na kwa wakati kwa njia ya barabara.
“Mhe. Waziri kwakweli sisi wananchi wa Kigoma Vijijini tunakushukuru sana sana, kwa kuliwezesha hili, tunampongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha Wanakigoma, tulikuwa tunateseka sana, tukilazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 50 kufuata huduma za kiserikali na kitabibu, lakini kwa ujenzi wa daraja hili la Bweru sasa tunasafiri umbali wa kilometa mbili, kutoka kwenye makazi yetu mpaka zilipo huduma muhimu za kiutawala na kijami”. alisema Mhe. Joseph Nyambwe.
Kwa mujibu wa Meneja wa TARURA wilaya ya Kigoma Mhandisi Elias Muttapima ujenzi wa daraja hilo unafungua njia kwa wakazi wa kata za Kagongo, Bweru, Bitale na Mahembe kwa kuwaunganisha na barabara za Mwandiga , Manyugu pamoja na Barabara ya Kasuru ambazo ni barabara muhimu katika shughuli za kibiashara, usafiri na usafirishaji wa mazao.