Naibu katibu wa wizara ya mifugo na uvuvi Dr Edwin Mhende akizungumza na wananchi wa kasanga mwambao wa ziwa Tanganyika.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Charles Makongoro Nyerere katikati wakati akikabidhi makasha ya kuhifadhia samaki
…………..
Na Neema Mtuka, Rukwa
Wananchi Wilayani Kalambo Mkoani Rukwa wametakiwa kuzingatia uvunaji unaofaa na kuachana na uvuvi haramu unaohatarisha kupotea kwa viumbe mbalimbali vinavyopatikana kasanga mwambao mwa ziwa Tanganyika.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu katibu wa wizara ya mifugo na uvuvi Dr. Edwin Paul Mhede wakati wa hafla fupi ya kukabidhi makasha ya kuhifadhia samaki.
Mhede amesema yapo mambo ya msingi yaliyopelekea ziwa hilo kufungwa Ambapo amezitaja sababu hizo kuwa ni kutunza mazalia ya samaki sambamba na kutunza rasilimali za nchi.
Awali akizungumza na wavuvi mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Makongoro Charles Nyerere amewataka wavuvi kuyatunza makasha ya kuhifadhia samaki lakini pia kuacha tabia ya uvuvi haramu.
Amesema uvunaji holela wa samaki ni kupoteza mazalia ya samaki hao na kusababisha kutoweka kwa viumbe hao.
“Hakikisheni mnafanya uvuvi endelevu na wenye tija utakaosaidia kuwapatia kipato na kujiinua kiuchumi.”Amesema Makongoro.
Aidha Mhede amesema wao kama wizara wamejipanga kuja na teknolojia za makasha kadiri mazao hayo yatakavyozidi kukua na watahakikisha wavuvi wengi wanafikiwa.
Baadhi ya wananchi ambao ni wavuvi wameiomba Serikali kuwapa mikopo ili wakati mwingine ziwa linapofungwa waweze kufanya shughuli nyingine za kujiingizia kipato kwani hawana kazi yoyote ya kufanya isipokuwa ni uvuvi.
Amesema uvuvi imekuwa sekta muhimu ambayo imeajiri zaidi ya watanzania mill 6 ambao ni sawa na asilimia 10 ikiwa kwa kipindi Cha miaka 10 iliyopita vyombo vya uvuvi vimeongezeka kwa asilimia 7.
Kupumzishwa kwa shughuli za ziwa Tanganyika zilianza rasmi Mei 15 Hadi Agost 15 2024 yakiwa ni makubaliano ya kimkataba baina ya nchi zinazotumia ziwa Tanganyika zikiwemo Zambia ,Rwanda, Burundi Kongo na Tanzania ili kuruhusu samaki na viumbe wengine wa majini kuzaliana kwa wingi na kukua hivyo kuwezesha rasilimali za uvuvi kunufaisha idadi kubwa ya wananchi.