NA JOHN BUKUKU, HARARE ZIMBABWE.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa kuchaguliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC -Organ Troika Summit) Taifa la Tanzania limepata heshima kubwa, huku akieleza kuwa ni fursa kwa wafanyabiasha kuzalisha bidhaa na kuuza katika Jumuiya hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 17, 2024 kando ya Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC) kuhusu masuala mbalimbali yaliyojadiliwa katika mkutano huo unaofanyika katika Jengo la Bunge la Zimbabwe (New Parliament Building) lililopo Kilima cha Mount Hapdeo jijini Harare, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Kombo, amesema kuwa Tanzania imekuwa ikitoa mchango mkubwa ndani ya SADC.
Balozi Kombo amesema kuwa Tanzania katika ukanda wa Nchi za SADC inaheshimiwa kutokana na kuwa miongoni mwa Nchi tatu zinazotoa mchango mkubwa ikiwemo kuchangia majeshi pamoja bajeti.
Amesema kuwa kuna biashara zinaendelea ndani Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika ambapo hadi kufikia sasa imefika asilimia 28.
“Tanzania itanufaika katika masuala ya uchumi kwani kwa sasa mtanzania hahitaji visa kwenda Nchi yoyote ukanda wa nchi za SADC” amesema Balozi Kombo.
Ameeleza kuwa pia kuna faida ya ulinzi na usalama pamoja na kufunguliwa milango ya kufanya biashara katika mazingira rafiki ndani ya SADC.
Akizungumzia mambo yanaendelea katika mkutano wa SADC, amesema kuwa Rais Dkt. Samia amepata nafasi ya kuongoza kikao cha SADC – Organ Troika Summit, huku akieleza kuwa kazi kubwa kwenda kutatua changamoto zilizopo katika jumuiya hiyo katika nchi mbalimbali ikiwemo Msumbuji na Kongo.