Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa Dkt.Venance Mwasse akiwa katika kikao kazi na Meneja Mkuu wa Kiwanda ya Neelkanth Lime Ltd Bw. Benny P. Pathrose, Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Wanawake Mkoa wa Tanga B. Mariam Mshana pamoja na Kaimu Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tanga Mhandisi Jackson R. Shirima wakati alipofanya ziara Leo Agosti 16, 2024 katika kiwanda hicho kilichopo Mkoani Tanga.
………….
Katika kuhakikisha Wachimbaji Madini Wanawake Mkoa wa Tanga wananufaika na Raslimali ya madini ya viwandani ya Chokaa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limejipanga kutengeneza mazingira rafiki ili waweze kuyafikia masoko na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza leo Agosti 16, 2024 Mkoa Tanga katika kikoa kazi kilichowakutanisha wachimbaji wa madini na Meneja Mkuu wa kampuni ya Neelkanth Lime Ltd, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt.Venance Mwasse, amesema kuwa
dhamira ya Serikali na Shirika ni kuona wachimbaji Madini hasa Wanawake wananufaika na shughuli ya uchimbaji ili kujikwamua kiuchumi.
Dkt. Mwasse amesema kuwa
Mkoa wa Tanga na wachimbaji wa madini wanapata changamoto ya kulifikia soko la kiwandani moja kwa moja na kusababisha kunyonywa na wanunuzi wa kati, huku akitoa wito kwa Meneja wa Kiwanda hicho kuwapa nafasi wachimbaji wanawake ili waweze kuuza Madini yao ya Chokaa kiwandani.
“Wanawake ni jeshi kubwa hivyo ukimkomboa mwanamke umeikomboa jamii kwa jumla hasa ukizingatia takwimu za sensa ya watu na makazi kwa Mwaka 2022 idadi ya kina mama ni kubwa ikilinganishwa na kinababa, tukifanya kazi kwa pamoja na kuwasaidia kina mama italeta mapinduzi makubwa katika kuboresha maisha ya watanzania.”amesema Dkt. Mwasse.
Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Neelkanth Lime Ltd, Bw. Benny P. Pathrose, amesema kuwa shughuli mbalimbali zinazofanyika kiwandani zinaleta fursa ya kufanya biashara za Madini, huku akisisitiza umuhimu wa kutatua changamoto zilizopo katika soko katika Mkoa wa Tanga.
Meneja huyo ametoa fursa kwa Wanawake wachimbaji Madini Mkoa wa Tanga wa kuuza tani 200 kwa siku za Madini ya Chokaa katika kiwanda hicho pamoja na kuwalipia Mirabaha yote ya madini watakayouza kiwandani hapo.
Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Wanawake Mkoa wa Tanga B. Mariam Mshana, amepokea kwa furaha nafasi hiyo waliyoipata ya kuuza Madini ya Chokaa kiwandani hapo, kwani itawawezesha kujiongezea kipato maradufu tofauti na hapo awali walikuwa wanapunjwa kupitia madalali
Katika ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa Dkt.Venance Mwasse ameambatana na Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Wanawake Mkoa wa Tanga B. Mariam Mshana pamoja na Kaimu Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tanga Mhandisi Jackson R. Shirima.