NA FAUZIA MUSSA
WAKALA wa Chakula na Dawa , Zanzibar (ZFDA) imeyafungia maduka manne ya bidhaa za nyama (mabucha) kutokana na kwenda kinyume na taratibu za kuendeshea biashara hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa bidhaa za mifugo Dk.Thamra Khamis Talib alieleza hayo mara baada ya kufanya ukaguzi katika maduka yaliopo maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema Taasisi hiyo inaendesha zoezi hilo mara kwa mara na kuchuka hatua mbalimbali kwa maduka ambayo yatabainika kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa na wakala huo ili kuhakisha bidhaa hizo zinabaki kuwa salama kwa matumizi ya binaadamu.
“Tunafanya ukaguzi huu ili kuhakikisha maduka yote ya nyama yanasajiliwa, yapo katika hali ya usafi, vifaa wanavyotumia ni sahihi ikiwemo misumeno ya moto na kuangalia afya za wahudumu wa maduka hayo kwa Lengo la kumlinda mtumiaji wa bidhaa hiyo, ” alifahamisha Dk.Thamra
Aidha aliwataka wafanyabiashara kufuta miongozo inayotolewa na wakala huo ikiwemo kupima afya, kusajili maduka na kudumisha usafi ili kumlinda mtumiaji wa mwisho wa bidhaa hiyo.
Alifahamisha kuwa licha ya juhudi wanazozichukua lakini bado wapo baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa hiyo wanaokwenda kinyume na utaratibu wa ZFDA jambo linalohatarisha afya za wananchi.
“Kati ya mabucha 15 – 20 tunayoyapitia ni mabucha matatu mpaka manne ndio yanayokidhi vigezo na masharti ya ZFDA” alieleza
Alisema hali hiyo inatokana na uelewa mdogo wa wafanyabiashara hao kwani wengi wao wanaangalia kipato na sio afya za watumiaji.
Aidha alieleza kuwa ZFDA itaendelea kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote wanaokwenda kinyume na taratibu za taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuyafungia maduka yao hadi pale watakapofuata taratibu hizo.
Mbali na hayo aliwataka wafanya biashara hao kufika ZFDA kupata elimu na miongozo ya ya kuendesha biashara hiyo ili kuepuka kuingia makosani.
Baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa hiyo akiwemo Juma Ali Vuai wa Kibandamaiti na Sleiman Hamad wa Jang’ombe waliahidi kufuata taratibu katika makosa waliobainika kuwa nayo ili kuwa salama katika kazi zao.
Miongoni mwa watumiaji wa bidhaa hiyo Mafunda Said Ali aliwashauri wafanyabiashara hao kuwa wazalendo na kujali afya za watumiaji badala ya maslahi binafsi na kuwasisitiza kudumisha usafi kwani ndio kivutio kikubwa cha wateja .
Hata hivyo walisema jukumu la kulinda afya linaanza kwa mtumiaji mwenyewe hivyo waliwashauri watumiaji kuangalia usafi wa muuzaji ,mazingira ya bidhaa yenyewe kabla ya kununua ili kulinda afya zao.
“Tunze kuzijali afya zetu sisi wenyewe tuhakikishe tunanunua bidhaa katika maduka ambayo ni masafi, wauzaji wake ni wasafi ili kulinda afya zetu, na hii inaweza kusaidia baadhi ya wafanyabiashara kubadilika na kudumisha usafi” alieleza
Katika ukaguzi huo ZFDA wamekagua maduka ya nyama maeneo ya Mombasa,Jang’ombe ,Amani, Magomeni na Kibandamaiti.