Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza James Ruge akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza James Ruge akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi zao kwa kipindi cha miezi mitatu kwa waandishi wa habari .
………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza imewezesha zaidi ya milioni 290 kukusanywa na Halmashauri za Mkoa huo na kuwasilishwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiwa ni makusanyo ya kodi ya zuio.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 16, 2024 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza James Ruge wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi zao kwa kipindi cha miezi mitatu kwa waandishi wa habari.
Amesema kazi hiyo ilifanyika kwa lengo la kuboresha na kuimarisha matumizi ya stakabadhi za EFD na ukataji wa kodi ya zuio kwenye manunuzi ya vifaa na huduma katika Halmashauri za Mkoa huo ili kuwezesha Serikali Kuu kukusanya mapato yake.
“Matokeo hayo yametokana na maazimio yaliyowekwa baada ya uchambuzi wa mfumo uliofanywa na TAKUKURU ukihusisha Halmashauri za Mkoa wa Mwanza na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)”, amesema Ruge
Akizungumzia mapungufu yaliobainika amesema ni baadhi ya Halmashauri kutokukusanya Kodi ya zuio kutoka kwa wazabuni na watoa huduma,baadhi ya watoa huduma hawatoi risiti za EFD wanapofanya biashara na Halmashauri,uelewa duni wa sheria ya kodi miongoni mwa watoa huduma na wapokea huduma pamoja na mifumo ya Halmashauri na TRA kutosomana”, amesema.