Na Mwandishi wetu, Mpapura
Upatikanaji wa Kitambulisho cha Taifa umekuwa changamoto kubwa hali inayopeleka Wafanyabiashara baadhi kushindwa kulipa kodi.
Ili Mfanyabiashara aweze kupata leseni ya biashara ni lazima awe na kitambulisho ama namba ya kitambulisho cha Taifa ambacho baadhi yao hawana na hivyo kushindwa kukata leseni na kuomba urahisi wa wao kupatiwa vitambulisho vya Taifa.
“Tunapenda sana kulipa Kodi, tatizo kubwa vitambulisho vya Taifa, tunaomba hivi vishushwe mpaka ngazi za chini tuvipate kwa wepesi na kwa haraka ili tuweze kusajilia biashara zetu.” alisema Halima Dadi mkazi wa Kijiji cha Mbuo.
Hayo yamejili kwenye ziara ya kusikiliza na kutatua kero za Wafanyabiashara iliyofanywa na Afisa Tarafa Mpapura Emmanuel Shilatu kwenye Kata zote za Tarafa akiambatana na Maafisa biashara na Kodi.
Afisa Biashara na Uwekezaji Alfred Mtawali aliwasisitiza Wafanyabiashara kukata leseni huku Afisa Kodi Ikrah Songoro akisisitiza kuwa TIN namba inatolewa bure kabisa na ni haki kwa Kila Mtanzania mwenye umri wa zaidi miaka 18 kuwa nayo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti Gavana Shilatu alisisitiza Kila Mtanzania mwenye sifa atapata Kitambulisho cha Taifa.
“Napenda niwahakikishe Kila Mtanzania mwenye sifa ukiwemo wewe Mfanyabiashara utapata Kitambulisho cha Taifa kilichoboreshwa. Na wale ambao vitambulisho vyao vimeshafika waende wakafichukue vitambulisho vyao.” Alisema Gavana Shilatu
Gavana Shilatu aliwasisitiza Wafanyabiashara kulipa Kodi ambayo husaidia kupeleka huduma na maendeleo kwao, hivyo Kodi wanayolipa ni maendeleo yao.
“Ni lazima tuelewe Serikali inapata nguvu ya kujenga miundombinu, kutoa huduma za afya na elimu na mengineyo ni kwa sababu ya kodi wanazolipa na tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyozisimamia Kodi kuhakikisha zinaleta matokeo chanya ya kimaendeleo kwa Taifa.” Alisema Gavana Shilatu.
Katika ziara hiyo ya kutoa elimu kusikiliza na kutatua kero za Wafanyabiashara na Wajasiriamali iliyofanyika kwa maeneo ya Kata zote za Tarafa ya Mpapura, Gavana Shilatu aliambatana na Maafisa biashara na Kodi.