Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akishiriki katika mkutano wa mawaziri wa Asasi ya ushirikiano ya ulinzi na usalama katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) wakishiriki katika mkutano huo.
Picha ya pamoja
Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na Dkt. Faustine Ndungulie kwenye uwanja wa ndege wa Robert Mugabe jijini Harare leo amempigia debe kwenye kikao cha mawaziri.
…………………
Na John Bukuku -Harare Zimbabwe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema Tanzania inalipa kipaumbele suala la kuimarisha ulinzi na usalama katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Amesema katika kufanikisha hili Tanzania inashiriki kikamilifu katika juhudi za kutafuta amani ndani ya kanda, barani Afrika na duniani ikiwa ni pamoja na kuchangia gharama zake.
Balozi Kombo ameyasema hayo Agosti 16, 2024 wakati akichangia hoja katika kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa katika masuala ya amani na usalama wakati wa Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO)
Mkutano huo umefanyika nje kidogo ya jiji la Harare katika Jengo jipya la Bunge la New Parliament Building eneo la kilima cha Mount Hapdeo Harare Zimbabwe Agosti, 16 2024. ambapo ameongeza kuwa Tanzania inaamini kuwa uzoefu wake utaiwezesha kuchangia kwa ufanisi katika jukumu la Baraza la Usalama
Waziri Kombo pia amewasilisha ombi la Tanzania kuendelea kuungwa mkono na nchi za SADC katika nafasi mbalimbali zinazowaniwa na Watanzania ikiwemo nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) – Afrika inayowaniwa na Dkt. Faustine Ndugulile.
Katika hatua nyingine ameomba Tanzania kuungwa mkono pia katika nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2026 – 2028 na Ujumbe usio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2029 na 2030.
Mkutano huo ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 15 Agosti, 2024 ambapo, mikutano hii miwili ni mikutano ya awali ya maandalizi ya agenda na nyaraka kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika leo tarehe 16 Agosti, 2024 ambapo kesho Agosti 17 katika mkutano wa wakuu wa nchi na viongozi wa serikali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan atapokea uenyekiti kuwa Mwenyekiti wa asasi hiyo.
Agenda zilizojadiliwa na mkutano huu ni pamoja na Hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda, Uimarishwaji wa Demokrasia katika Kanda, Mfumo wa Kuwaenzi Viongozi Waasisi wa SADC na Wagombea wa Nafasi mbalimbali wa Kanda katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa.
Mkutano huo pia umehudhuriwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW).
Jengo jipya la Bunge la New Parliament Building eneo la kilima cha Mount Hapdeo Harare Zimbabwe linavyoonekana kwa mbele
Hii ni moja ya barabara inayoonekana kwa chini ukiwa kwa nje kwenye jengo hilo ka bunge.
Moja ya majengo uanayolipamba jiji la Harare.