Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amekutana na
kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald
Lamola na Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Mhe. Dkt. Rasata Rafaravavitafika
pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) leo tarehe 14 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.
Akizungumza na Mhe. Lamola,
Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano wa
kihistoria na kindugu uliopo baina ya Tanzania na Afrika kusini ili kukuza
sekta za kiuchumi ikiwemo biashara, utalii, uwekezaji, elimu, afya na maeneo
mengine ya kimkakati kwa maslahi ya pande zote mbili.
Naye Mhe. Lamola ameeleza kuwa
Afrika Kusini inaendelea kuthamini mchango wa Tanzania katika harakati za
ukombozi wa Taifa hilo hivyo, ina nia ya dhati ya kuuenzi mchango huo kwa
kukuza ushirikiano katika shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa ustawi
wa wananchi wa mataifa hayo mawili.
Aidha, katika mazungumzo ya Mhe.
Kombo na Mhe. Dkt. Rafaravavitafika wamejadili juu ya kuendelea kuimarisha
ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi na taifa hilo hususan katika sekta ya
uchumi wa blue ambao Tanzania imeuwekea mkazo ili kukuza uchumi kupitia
rasilimali za bahari zinazopatikana na kukuza biashara yake kimataifa.
HABARI
KATIKA PICHA: Waziri
Kombo alipokutana kwa mazungumzo na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola.