Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dastan Kitandula akiwa na Katibu wa Kamati ya CPC ya Utawala wa Forodha ya Watu wa China Yu Jianhua wakisaini ya Itifaki ya Kuuza ya Asali ya Tanzania nchini China katika hafla iliyofanyika leo Agosti 15, 2024 jijin Dar es Salaam
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali ya Tanzania na China zimeingia makubaliano na kuuza asali ya Tanzania nchini China ambayo kila mwaka inaagiza nje ya nchi zaidi ya tani za Asali milioni 38.
Akizungumza leo Agosti 15, 2024 jijini Dar es Salaam katika hafla ya Uwekaji saini Itifaki ya kuuza Asali ya Tanzania nchini China, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dastan Kitandula, amesema kuwa wakati umefika kwa watanzania kuchangamkia fursa ya kuzalisha asali yenye ubora kwa wingi ili kuinua vipato vyao na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Mhe. Kitandula amesema kuwa mkataba huo unakwenda kuondoa kikwazo kilichokuwepo hapo awali na kukidhi haja ya wafanyabiashara wa Tanzania ya kuuza asali katika masoko ya China.
Mhe. Kitandula amesema kuwa kufunguka kwa soko la asali nchini China kunaenda pamoja na kutekeleza masharti kadhaa yaliyobainishwa kwenye itifaki.
“Moja ya sharti ambalo wafanyabiashara wenye nia ya kuuza asali nchini China, nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani wanapaswa kutekeleza ni kuhakikisha kuwa Kampuni zao zinasajiliwa kwenye Mifumo ya Kimataifa ya Udhibiti wa Afya na Usalama wa Vyakula; Afya ya Mimiea; na Ulinzi wa Mazingira” amesema Mhe. Kitandula
Amefafanua kuwa usajili wa Wafanyabiashara/Makampuni katika Mifumo hufanyika kwa njia ya kidigitali na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambapo kuna dawati maalum kwa ajili ya kusaidia Wafanyabiashara kujisajili na kutoa rai kwa makampuni ambayo bado hayajasajiliwa yasajiliwe.
Amesema kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafugaji nyuki na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki kwa kutoa Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani VAT kwa vifaa na mashine mbalimbali zinazohusiana na ufugaji nyuki na kuongeza thamani mazao ya nyuki.
Mhe. Kitandula amesema Serikali imejenga viwanda sita vya kuchakata mazao ya nyuki katika Wilaya za Kibondo, Sikonge, Mlele, Nzega, na Bukombe ili kuhakikisha kuwa asali inayouzwa nje ya nchi inakuwa na viwango vya ubora vinavyokidhi mahitaji ya masoko hayo.
Tanzania ina uwezo wa kuzalisha takribani tani 138,000 za asali kwa mwaka, kwa sasa uzalishaji wa asali upo kwenye kiwango cha takribani tani 33,276 sawa na asilimia 24.1 ya uwezo uliopo.
Kiwango hiki kinaiweka Tanzania katika ramani ya Dunia na kuifanya kuwa nchi ya Kwanza kwa uzalishaji wa asali katika nchi za Afrika Mashariki na SADC; nchi ya Pili kwa uzalisahji wa asali barani Afrika; na nchi ya 14 Duniani kwa uzalisahji wa asali.
Hii inaonyesha kuwa sekta ya ufugaji nyuki ni muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na ina nafasi kubwa ya kuendelea kukua na kuchangia zaidi katika Pato la Taifa na ajira kwa wananchi.