Na Sophia Kingimali.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila amelipongeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini(TPDC) kwa kuendelea na kuwajengea uwezo makundi mbalimbali nchini kuhusu utunzaji wa miundombinu ya shirika hilo.
Pongezi hizo amezitoa leo Agosti,15 2024 jijini Dar es Salaam Chalamila wakati akifungua semina ya viongozi wa dini,madiwani na wadau mbalimbali iliyoandaliwa na TPDC kwaajili ya kuwajengea uwezo na kuwa mabalozi wazuri katika ulinzi wa miundombinu ya usafirishaji wa gesi, mafuta pamoja na mambo mengine.
“Agenda kubwa ya semina hii ni kuwajengea uwezo ili mkawe mabalozi wazuri kwa wananchi wanakoishi kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu ya TPDC kwani Miundombinu hii ina manufaa makubwa kwa nchi na kwa wananchi kwani inasaidia kusafirisha gesi kwenda kwa watanzania au kwenda kwa walaji,” amesema Chalamila.
Amesema TPDC wanapaswa kuendelea kufanya semina hizo kila mara ili kuweza kuongeza uelewa kwa jamii katika maeneo ambayo kuna miundombinu yao imepita kwani inaweza kuharibiwa na watu wenye uelewa mdogo.
Aidha amewataka Viongozi wa dini wakatumie misikiti Makanisa kupeleka ujumbe kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa kutunza miundombinu hiyo lakini umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia katika utunzaji wa mazingira lakini kulinda afya.
Chamila amesema shirika hilo ambalo linatekeleza miradi yake mingi ikiwemo miradi mkubwa wa lindi kusafirisha gesi na miradi mingine ambayo inatekelezwa katika miradi hiyo moja wapo kuna njia za usafirishaji wa gesi.
Amesisitiza umuhimu wa kutumia nishati safi TPDC wakiwa na miundombinu ya kusafirisha gesi asilia gesi hiyo kusaidia kutumia majumbani, magari viwandani na maeneo mengine bila kutumia na kuepuka nishati chafu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Francis Mwakapalila amesema lengo la semina hiyo kupata fursa ya kujifunza na kuongeza uelewa kuhusu gesi asilia lakini pia kukumbushana majukumu ya kuhusu shirika hilo.
Ameongeza kuwa Jukumu la msingi la shirika hilo kufanya tafutaji, uendelezaji na usafirishaji wa gesi asilia
“Utekelezaji wa miradi ya kimkakati jumla ya miradi 19 ambapo miradi tisa ipo chini ya Wizara ya Nishati na miradi minne ipo chini ya TPDC ambayo ni gesi LNG, ECO bomba la kusafirisha mafuta ambalo limepita mikoa nane, utafutaji mafuta na utafutaji gesi asilia,” amesema.
Ameongeza kuwa TPDC imebuni miradi mbalimbali ikiwemo ya gesi asilimia ambapo asilimia 57 ya umeme unaozalishwa kwenye Gridi ya Taifa unatokana na gesi asilia.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya amani Kinondoni, Majaliwa Selemani amesema semina hiyo imekuja wakati muafaka kwani itawasaidia kujua namna ya kutunza miundombinu hiyo kwani serikali imewekeza gharama kubwa.
“Serikali kwa kutambua mchango wetu katika jamii kwa sababu asilimia kubwa watu hawa tunaishi nao hivyo tunatoa elimu kwa mtu mmoja mmoja kulinda miundombinu ya gesi asilia kwa faida yetu na Taifa kwa ujumla,”amesema.
Semina hiyo imewakutanisha viongozi wa dini na madiwani wa mkoa wa Dar es Salaam katika Wilaya ya Ubungo, Kinondoni, Ilala na maeneo mengine.