Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Jaffari Matundu, akizungumza na wafanyakazi wakati wa hafla ya maadhimisho ya Miaka 27 ya benki hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997. Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ‘Miaka 27 ya Kukupa Kipaumbele’ yamefanyika katika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam tarehe 15 Agosti, 2024.
Mkuu wa Kitengp cha Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Stanley Kafu akizungumza katika sherehe za kuadhimisha Miaka 27 ta benki hiyo tangu kuanzishwa kwake. Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ‘Miaka 27 ya Kukupa Kipaumbele’ yamefanyika katika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam tarehe 15 Agosti, 2024.
Dar es Salaam: Benki ya Exim Tanzania imeadhimisha miaka 27 tangu kuanzishwa kwake katika safari iliyojaa mafanikio, ubunifu, na huduma bora kwa wateja wake. Ikiwa na kaulimbiu ‘Miaka 27 ya Kukupa Kipaumbele’, inaangazia mafanikio yake na mikakati madhubuti ambayo imejiwekea ili kuendeleza mafanikio hayo miaka mingi ijayo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Jaffari Matundu, alielezea baadhi ya mafanikio makubwa ambayo benki imefikia tangu kuanzishwa mwaka 1997.
“Miaka 27 iliyopita, tulianza safari ya kubadilisha sekta ya benki nchini na leo tunajivunia kuwa miongoni mwa watoa huduma bora wa kifedha. Mpaka sasa tumevuka mipaka tukiwa na matawi katika nchi tatu za Comoros, Djibouti, na Uganda,” alisema Matundu.
Dhamira ya Exim Bank ya ubunifu imekuwa nguzo kubwa katika mafanikio yake. Mfano, hivi karibuni, benki hiyo ilitunukiwa tuzo ya “Chapa ya Benki Yenye Ubunifu Mkubwa Tanzania – 2024” inayotolewa na jarida maarufu duniani la International Business Magazine ikiwa ni ushahidi wa huduma bora zinazotolewa na benki hiyo. Uboreshaji wa hivi karibuni wa mfumo wake wa Kibenki (CBS) ni sehemu ya mikakati ya Exim Bank kuboresha na kuongeza uharaka wa miamala, usahihi, na huduma bora kwa wateja kiujumla.
Mwaka 2023, Benki ya Exim ilipata mafanikio makubwa ya kifedha, ikiwa na faida kabla ya kodi ya TZS bilioni 91.5, uwekaji wa fedha za Wateja kufikia TZS trilioni 2.4, na jumla ya mali ikivuka TZS trilioni 3. Mafanikio haya yanaonesha kiwango cha uaminifu wa benki ya Exim kwa wafanyakazi na imani kwa wateja wake.
Benki ya Exim itaendelea kukua na kujipambanua zaidi kuongeza wigo na kufikia maeneo zaidi ndani na nje ya Tanzania. “Tutaendelea kuwa wabunifu, kutafuta namna bora zaidi za kutoa huduma kwa wateja wetu na hivyo kuchangia katika maendeleo ya sekta ya kifedha. Tuna malengo ya kuboresha ufanisi wa utendaji wetu, huduma kwa wateja, na bidhaa tunazotoa, kuhakikisha Exim Bank inaendelea kuwa kinara katika sekta ya kibenki nchini,” aliongeza Matundu.
Stanley Kafo, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Exim Bank, akielezea kuhusu safari yao, “Tunajivunia timu yetu kwa kazi nzuri na wateja wetu wote. Ni jambo la faraja kujua kwamba tunachangia katika ukuaji na kuboresha maisha ya Watanzania kote nchini.”
Benki ya Exim inaposherehekea mafanikio haya, Matundu alitoa shukrani kwa wateja, wanahisa, wafanyakazi, na washirika wa benki hiyo. “Msaada wenu kila wakati umechangia katika mafanikio haya. Tunahaidi kuendeleza safari yetu ya ubora, ubunifu, na ukuaji, kuhakikisha Benki ya Exim inabaki kuwa mstari wa mbele katika sekta ya benki nchini,” alihitimisha.