*Wasema si vizuri anavyobaguliwa ‘ulaji’ wa ruzuku na kunyimwa haki ndani ya Chadema
*Wachanga fedha atengeneze gari moja mbovu analotumia_
*Wakati yeye akitumia gari moja na wenzake 8, Mbowe ana msafara wa magari 15 na chopa juu ambazo ni fedha za ruzuku
Maelfu ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa sehemu ya mkutano mkubwa wa hadhara uliohutubiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, wamemchangia Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Ndugu Tundu Lissu mamilioni ya fedha ili amudu kutengeneza gari yake anayotumia kwenye shughuli zake mbalimbali.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa mbalimbali, ambazo pia zimewahi kumnukuu yeye mwenyewe Lissu akilalamika kuwa hatendewi haki na anadhalilishwa ndani ya Chama chake hicho kwa yeye kutumia gari moja mbovu, inayombeba pamoja na walinzi wake wanane, huku Mwenyekiti wake Freeman Mbowe akiwa na msululu wa magari 15 ardhini na helkopta angani.
Hayo pia yamejiri siku chache baada ya Kada wa CCM, Mchungaji Peter Simon Msigwa, aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, kusema hadharani kuwa Lissu ananyanyaswa na kubaguliwa katika chama hicho kiasi cha kunyimwa stahiki nyingi zinazohusu nafasi yake akiwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, ambapo mbali ya usafiri, hata fedha za kujikimu yeye na watu anaokuwa nao hapati, huku akilazimika pia kutumia majukwaa ya mikutano yasiyokuwa imara na hatarishi kwa hali yake, huku Mwenyekiti wake akitumia majukwaa yanayotengenezwa kwa gharama kubwa kila anakokwenda.
Mchango huo uliofikia shilingi milioni tano, umekusanywa kwenye mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Furahisha, jijini Mwanza, leo Agosti 15, 2024, ukiwa ni hitimisho la ziara ya siku mbili ya Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Nchimbi, katika Mkoa wa Mwanza, akiwa pia amehitimisha ziara ndefu aliyoanzia Mkoa wa Kigoma, kisha Kagera, Geita na hatimae Mwanza.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC), Ndugu Amos Gabriel Makalla, aliyeendesha shughuli hiyo ya kuchangisha mchango huo, alitangaza kiasi kilichopatikana kuwa ni Sh. 5,320,000, na akaongeza kusema fedha hizo taslimu zitawekwa kwenye akaunti ya benki ya mwanasiasa huyo, baada ya Mchungaji Msigwa kuthibitisha kuwa anayo akaunti hiyo.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Nchimbi amehitimisha ziara yake ya siku 15 katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita na Mwanza ambayo ilikuwa na malengo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025, kukagua uhai na uimara wa CCM, pia kuzungumza na kuwasikiliza wananchi katika maeneo yao.
Katika ziara hiyo, ambayo pia mafanikio yake imekuwa ni pamoja na kuendelea kurejesha na kuvuna wanachama wa vyama vingine, wanaorejea kujiunga CCM kutokana na kazi nzuri zinazogusa wananchi zinazofanywa na Serikali ya CCM, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Balozi Nchimbi aliambatana na Katibu wa NEC – Oganaizesheni, Ndugu Issa Haji Usi Gavu, Ndugu Makalla (Mwenezi) na Katibu wa NEC – Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndugu Rabia Hamid Abdalla.