Jaji rufaa mstaafu,Eusebia Munuo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha.
………..
Happy Lazaro,Arusha.
Mtandao wa kupinga rushwa ya ngono Tanzania wameiomba serikali kutofanyiwa marekebisho ya sheria ya kupinga rushwa ya ngono yaliyobainishwa kwenye kifungu cha 10(b)cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Hayo yamebainishwa mkoani Arusha na Jaji rufaa mstaafu,Eusebia Munuo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha ambapo amesema kuwa endapo sheria hiyo itafanyiwa marekebisho
italenga kumlinda mhalifu badala ya kuwa msingi wa kuzuia uhalifu na kulinda haki.
Munuo amesema kuwa,kifungu cha 25 kibaki kama kilivyo na kiendelee kutumika kwani kinajitosheleza bila kumbagua mhalifu awe wa kike au wa kiume.
Aidha wameomba bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania lisipitishe haya mabadiliko kwani kazi ya Bunge ni kutunga sheria za kulinda haki na sio kutunga sheria ya kumlinda mhalifu ,huku wakitoa wito kwa watanzania wote pamoja na watetezi wa haki za binadamu hususani wanawake na watoto wa kike kupinga vitali kuingizwa kwa kifungu cha 10(b) kwenye huu muswada.
Nao baadhi ya wanamtandao hao wakizungumzia kuhusiana na mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya ngono wamesema kuwa, wanatambua mwitikio wa elimu ya kuzuia na kupinga rushwa ya ngono umekuwa mkubwa kwa wazazi,watoto mashuleni,vijana vyuoni,kwenye taasisi za kusini,waajiriwa majumbani na maofisini na katika tasnia ya sanaa na utamaduni.
Mkurugenzi wa shirika la MIMUTIE Women Organization ,Rose Njilo amesema kuwa wao wanatambua nyongeza ya kifungu cha 10(b) ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa ,sheria za kuzuia rushwa za SADC ,Umoja wa Afrika Afrika kanuni zote zinazoongozwa na Muungano wa Afrika Mashariki zinazokataza rushwa ya ngono.
Amesema kuwa, swala la rushwa ya ngono limekuwa ni changamoto kubwa sana katika jamii maana inadhalilisha Taifa na wengi wanaofanya vitendo hivyo ni maafisa wakubwa katika ofisi mbalimbali kwani wanaopata changamoto zaidi ni watu waliopo pembezoni, hivyo wamesikitika sana kuona kifungu hicho kinatolewa.
“Sisi wanamtandao unaopinga rushwa ya ngono hatukubaliani kabisa na marekebisho yaliyobainishwa kwenye kifungu cha 10(b) na tunapendekeza kifutwe kabisa kwani kinaenda kinyume kabisa na dhana nzima ya kifungu cha 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa na kinalenga kumlinda mhalifu badala ya kuwa msingi wa kuzuia uhalifu na kulinda haki. “amesema .
Mkurugenzi wa Dunia salama Foundation, Idd Ninga amesema kuwa, endapo bunge litapuuza madai yao,wanatoa wito kwa Rais Samia kukataa kuridhia haya mabadiliko yanayowasilishwa bungeni kwa kuwa athari zake ni kubwa sana kwa Taifa letu.
Aidha wanamtandao hao wametoa tamko hilo baada ya kufutwa kifungu cha nyongeza cha 25 (b) kilichompokonya mhanga haki na badala yake kuongeza kifungu 10(b) kinachohalalisha kuendeleza matumizi mabaya ya mamlaka kwa njia ya kumhukumu mhanga wa rushwa ya ngono kama mbinu ya kuwanyamazisha na kuzima moto mapambano dhidi ya rushwa ya ngono.