OR – TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ameitaja Kigoma kuwa miongoni mwa mikoa inayolegalega katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akiwataka watendaji kuongeza juhudu katika kutekeleza miradi mikubwa ya serikali na utoaji wa huduma kwa jamii.
Waziri Mchengerwa ametoa agizo hilo Agosti 12, 2024 wakati wa ziara yake mkoani Kigoma alipokutana na kuzungumza na watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo pamoja na watendaji wa taasisi mbalimbali za umma ngazi ya mkoa na wilaya.
Waziri Mchengerwa amesema wananchi wana kiu kubwa ya maendeleo wakitamani kuona miradi inayotekelezwa katika maeneo yao inakamilika kwa wakati hivyo watendaji hawana kisingizio chochote cha kuchelewesha miradi hiyo.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia OR – TAMISEMI analeta fedha za kutosha kutekeleza miradi yote nchi nzima, sisi watendaji hatuna namna yoyote ile tunayoweza kusema kwa nini tunalegalega katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo” alisema Waziri Mchengerwa.
Ameongeza kuwa Ofisi yake haitamvumilia mtendaji yeyote anayelegalega katika kipindi chake akisisitiza uwajibikaji kwa jamii na utatuzi wa kero za wananchi kuwa kipaumbele namba moja kwa watendaji wake.
“Mimi na Wakurugenzi tumekubaliana miradi yote inayohiusu OR- TAMISEMI iwe imekamilika kufikia Desemba 30, 2024, na kwenye hili Wakuu wa Wilaya simamieni, fuatilieni kwa ukaribu miradi hii ni ya kwenu, sasa tukisikia miradi haijakamilika maana yake na nyinyi mnahusika moja kwa moja tusiwaonee wakurugenzi peke yake” alisema Waziri Mchengerwa
Aliongeza kuwa “kuanzia sasa nataka niwaone mkiwa bega kwa bega kukagua kila mradi uliopo kwenye wilaya zenu na mtushauri maana taarifa zenu zitatusaidia sana kufanya maboresho kuliko taarifa tukizipata kienyeji na kupitia kwenye vyombo vya habari”.
Kadhalika Waziri Mchengerwa amewataka watendaji katika mamlaka yake kuwa msatari wa mbele kubainisha changamoto za maeneo wanayo yahudumia ili kuweka urahisi kwa viongozi wenye mamlaka kuzitafutia ufumbuzi.
Waziri Mchengerwa yuko mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo anatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa chini ya OR – TAMISEMI.