Na OR TAMISEMI, Kilimanjaro
Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Kiseo Yusuf Nzowa amefungua mafunzo kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wa mkoa huo na kuwataka waondoe changamoto zao kwa kutokuwa sehemu ya migogoro kwenye maeneo yao.
Bw. Kiseo Yusuf Nzowa ametoa kauli hiyo mapema leo tarehe 11 Agosti, 2024 katika ukumbi wa Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wa mkoa huo na kuwataka kuondoa changamoto zilizopo kwenye maeneo yao hususani migongano yao ya kiutendaji na migongano na jamii kwenye maeneo yao.
“nizitaje baadhi ya changamoto ambazo zipo, moja ni migogoro ya kiutendaji baina ya wataalam na Viongozi, au na wanasiasa katika maeneo yenu, unaweza ukakuta Mtendaji wa Kata haelewani na Afisa Tarafa wake, haelewani na mtu fulani, sasa hili ni tatizo kwa sababu huwezi kufanya kazi vizuri yenye mafanikio kwenye sehemu ambayo inachangamoto” alisema Bw. Kiseo Nzowa.
Aidha, Bw. Nzowa amewataka washiriki hao kuwa wabunifu na wadadisi ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwenye maeneo yao kwani Serikali bado inauhitaji mkubwa wa mapato kwa ajili ya kuhudumia wananchi ikiwemo miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa ambayo inahitaji fedha nyingi za Serikali ili ikamilike na kusisitiza kwamba ukusanyaji wa mapato ya Serikali ni roho na uti wa mgongo wa Tanzania.
Bw. Ibrahim Minja ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha utendaji kazi kwa washiriki hao kwa kuzingatia majukumu yao na mpaka sasa mafunzo hayo yapo katika awamu ya tano na jumla ya mikoa 24 imekwishafikiwa na mafunzo hayo ambapo imebaki mikoa miwili ya Tanga na Iringa.
Naye Bw. Hussein Ally Kadangu Afisa Mtendaji Kata ya Bombo Halmashauri ya Wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kupeleka mafunzo hayo mkoani Kilimanjaro na kuahidi kwa niaba ya washiriki wenzake kwenda kuyatekeleza yale yote ambayo watafundishwa katika siku mbili za mafunzo kwenye maeneo yao.
Mafunzo kwa Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa nchini yanatolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia Programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Regions and Local Government Strengthening Programme-RLGSP) kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo pamoja na Chuo cha Utumishi wa Umma na mpaka sasa jumla ya mikoa 24 imepata mafunzo.