Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Manyara, Peter Toima amesema hakuna chama mbadala zaidi ya CCM kwenye mkoa huo hivyo wanatarajia ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu wa 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka kesho 2025.
Toima ameyasema hayo akiwa mgeni rasmi katika kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro, wakati wa sherehe za Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer, ambapo amemsimika kuwa kiongozi wa kimila (Laigwanani).
Amesema watu wa Manyara wanaimani kubwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na uchapakazi wake hivyo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kura zote zitakuwa CCM.
Amesema kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa za mwaka huu wa 2024, CCM itashinda kwa kishindo kwenye nafasi za vitongoji, vijiji na mitaa na pia mwaka kesho 2025 kwenye udiwani, ubunge na Rais.
“Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka kesho 2025 hakuna mwana Manyara atakuwa ametoa kura yake kwa Rais, mbunge au diwani wa chama kingine zaidi ya CCM,” amesema Toima.
Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Manyara, akizungumza kwenye sherehe hizo baada ya kumsimika Taiko kuwa kiongozi wa kimila (Laigwanani) amempongeza kwa kupata nafasi hiyo.
“Tunakupongeza Taiko kwa kupata nafasi nyingine ya kuongoza jamii ya kifugaji kwani baada ya nafasi ya udiwani, umeongezewa pia nafasi nyingine ya kuitumikia jamii ya kiongozi wa kimila,” amesema Toima.