WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk.Seleman Jafo akizungumza na wafanyakazi wa Tume ya Ushindani FCC jijini Dar es Salaam leo Agosti 12, 2024.
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk.Seleman Jafo akimsikiliza Dkt. Agrey Mulimuka Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya FCC wakati alipozungumza na Menejimenti ya taasisi hiyo.
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk.Seleman Jafo akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa FCC wakati alipowasilisha maelezo mafupi kuhusu taasisi hiyo.
……………….
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk.Seleman Jafo amesema Wizara hiyo inafursa kubwa kutengeneza ajira kwa Watanzania kupitia sekta binafsi ikiwemo viwanda, hivyo watahakikisha wanatimiza azma hiyo ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuleta maendeleo kwa wanachi.
Waziri Dk.Jafo ameyasema hayo leo Agosti 12, 2024 Jijini Dar es Salaam, alipotembelea FCC kujitambulisha kwa viongozi wa Taasisi hiyo tangu ateuliwe na kuzungumza nao juu ya kazi kubwa wanayoifanya katika kulinda ushindani nchini.
Amesema Wizara hii ni pana na ina umuhimu mkubwa katika kutoa ajira kwa wananchi kupitia sekta binafsi, hivyo lazima tuhakikishe tunaweka mazingira mazuri kuongeza uwekezaji ambao unatoa ajira kwa Watanzania wengi.
Amesema kwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk.Samia, ndani ya miaka mitatu imechochea ongezeko la viwanda vikubwa kwa asilimia 27, ikiwa ni hatua kubwa ya ukuaji sekta hiyo na kuchochea ukuaji uchumi.
Dk.Jafo Amesema watahakikisha wanaongeza kasi ya kazi hiyo kubwa, ambayo imefanyika kutimiza azma ya Rais Dk. Samia ya kuvutia uwekezaji kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Katika hatua nyingine, Waziri Dk.Jafo amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na FCC katika kuchochea ongezeko la viwanda kwa kuwezesha miungano halali ya viwanda vya ndani na wawekezaji kutoka nje ya nchi.
“Mmefanya kazi kubwa na nzuri iliyowezesha serikali kupata mabilioni ya fedha, mpendane, mshirikine mfanye kazi kwa bidiii kuendeleza kazi hii muhimu. Pia, muhakikishe mnafanya ukaguzi kwa makampuni mbalimbali ikiwemo ya madini ambayo yameungana bila kufuata taratibu. ” Amesema Jafo
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa FCC, Dk. Agrey Mlimuka, amempongeza Waziri Jafo kwa kuwatembelea huku akiahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo yote aliyoyatoa ikiwemo la kufanya ukaguzi wa miungano ya makampuni.
Amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na FCC katika kuchochea ongezeko la viwanda kwa kuwezesha miungano halali ya viwanda vya ndani na wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa FCC Willium Erio amesema kuwa FCC inafanya kazi kubwa ya kuhamasisha ushindani halali nchini na kudhibiti bidhaa bandia kwa lengo la kulinda soko na kuvutia uwekezaji kwa kuweka mazingira bora ya biashara nchini.
Amesema katika kutekeleza hilo wamewezesha maboresho ya sheria kuendana na mazingira ya sasa, hali ambayo imesaidia kuunganisha kampuni na viwanda na kuchangia ukuaji wa uwekezaji nchini na kukuza uchumi.