Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke(TRRH) imezindua rasmi jengo la Huduma za Usafishaji Damu kwa wagonjwa wa figo, pamoja na gari la dharura maalumu kwa ajili ya mama na mtoto. Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 12 Agosti 2024, ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu.
Jengo hili jipya la usafishaji damu ni moja ya maboresho makubwa yaliyofanyika hospitalini hapo, hatua ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma za usafishaji damu kwa wananchi wanaoishi maeneo ya karibu na Temeke, hivyo kupunguza changamoto za kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mhe. Sixtus Mapunda ametoa salamu kutoka kwa Waziri wa Afya, zilizosisitiza umuhimu wa wananchi kujenga tabia ya kufanya mazoezi na kuzingatia ulaji bora wa vyakula ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, na matatizo ya afya ya akili, ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuwahimiza wananchi kufanya mazoezi na kupunguza ulaji wa vyakula visivyo na afya ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” alisema Mhe. Mapunda.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Dkt. Joseph Kimaro, ameeleza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na hospitali hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1970. Amesema kuwa hospitali hiyo imefanikiwa kufikia upatikanaji wa dawa muhimu kwa asilimia 98 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu. Aidha, ameongeza kuwa hospitali imeajiri watumishi 120 wa mkataba katika kada mbalimbali za afya ili kuboresha huduma, hususan huduma za kibingwa na bingwa bobezi.
Dkt. Kimaro ameendelea kwa kutoa shukrani kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kuchangia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa jengo la wodi ya usafishaji damu.
Aidha, uzinduzi huo umehusisha pia gari jipya la kubeba wagonjwa, ambalo litakuwa maalumu kwa ajili ya mama na mtoto. Gari hilo litasaidia sana katika kuwahisha kina mama wajawazito wanapohitaji huduma za dharura pamoja na kuwahudumia watoto kwa haraka na kwa usalama zaidi. Ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi na kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, kuhakikisha huduma bora na salama zinatolewa kwa wananchi.