Na Mwandishi wetu, Mirerani
MBUNGE wa Jimbo la Kiteto, Mkoani Manyara, wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau, amesema hakuna kipindi ambacho miradi ya maendeleo imetekelezwa kwenye majimbo mbalimbali kama kipindi cha uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Ole Lekaita ameyasema hayo kwenye kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro, wakati wa sherehe za Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer kusimikwa kuwa kiongozi wa kimila (Laigwanani).
Amesema Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, amefanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye majimbo kuliko kipindi cha uongozi wa Rais yeyote tangu nchi ipate uhuru.
Amesema miradi mingi ya maendeleo ya zahanati, vituo vya afya, hospitali, nishati ya umeme, fedha za barabara na shule hizo zote ni kazi nzuri ya Rais Dk Samia, ambavyo kama ilivyofanyika Kiteto, pia imefanyika na maeneo mengine.
“Hakuna wakati tumepata miradi mingi sana ya maendeleo kwenye majimbo kama kipindi hiki cha uongozi wa Rais Dkt Samia kwani kwenye kila jimbo kumefanyika maendeleo,” amesema Ole Lekaita.
“Mwenyezi Mungu ampe maono mazuri ili Taifa la Tanzania lizidi kusikika nchi za nje na sisi tuzidi kumuombea uzima na afya tele na mwakani 2025 kwenye uchaguzi mkuu tumpe kura nyingi za ndiyo,” amesema Ole Lekaita.
Hata hivyo, amempongeza Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer kusimikwa kuwa kiongozi wa kimila wa jamii ya kifugaji, ndiyo sababu naye akashiriki pamoja nao kwenye sherehe hizo.
“Sisi Kiteto na Simanjiro ni majirani na awali tulikuwa wilaya moja hivyo nimekuja kushiriki pamoja nanyi ili kuwaletea salamu nyingi kutoka Kiteto katika tukio hili la kiongozi wa kimila kusimikwa,” amesema Ole Lekaita.