Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Lenana Lenganasa Soipey ameitaka jamii ya wafugaji kutosikiliza maneno ya wanasiasa uchwara wanaoadaa umma kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inataka kuwapora ardhi wafugaji.
Lenganasa ameyasema hayo wakati akizungumza na jamii ya wafugaji kwenye kijiji cha Lengasiti Kata ya Naisinyai katika ziara ya Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka.
“Jamii ya kifugaji isipotoshwe na wanasiasa uchwara wanaoadaa umma kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itawapora ardhi yao na kugeuza kuwa mapori tengefu,” amesema Lenganasa.
Amesema wanasiasa hao uchwara ni dhahiri kuwa wanagombanisha wafugaji na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwani haiwezi kuleta maendeleo ya sekta ya elimu, afya, nishati ya umeme, maji na barabara kisha iwafukuze wafugaji.
“Wafugaji tuendelee kumuunga mkono Rais wetu mpendwa mama Samia na tusisikilize kelele za wanasiasa uchwara wanaopotosha jamii kuwa maeneo ya makazi na ya ufugaji yatageuzwa kuwa mapori tengefu,” amesema Lenganasa.
Hata hivyo, ametolea mfano eneo la milima ya Laletema kwani kwenye ramani ya miaka iliyopita inatambulika kuwa ni pori tengefu ila hadi sasa wafugaji wanatumia eneo hilo kwa malisho ya mifugo na shughuli nyingine hivyo wasipotoshwe.
Amewasihi wafugaji kuhakikisha kuwa kipindi cha uchaguzi mkuu mwaka kesho 2025 kikifika wampe kura nyingi za ndiyo Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuendelea kuwa Rais wa Tanzania kwani amefanya maendeleo mengi.
Amesema serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia inawapenda wafugaji ndiyo sababu ya kuwaletea maendeleo mengi hivyo wanapaswa kuendelea kuiunga mkono kwani inawajali.