NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, akizungumza na wataalamu wa banda la mradi wa kilimo cha Viungo Zanzibar (Agri-connet), katika maonyesho ya saba ya kilimo ya nane nane Zanzibar huko Dole Wilaya ya Magharibi “A” Zanzibar.
………………
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, ameishauri Wizara ya kilimo,umwagiliaji,maliasili na mifugo nchini kuendeleza utamaduni wa kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kufanya kilimo na ufugaji wa kisasa ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani la chakula.
Kauli hiyo ameitoa wakati akitembelea maeneo mbalimbali ya maonesho ya saba ya kilimo ya nane nane Zanzibar huko Dole Wilaya ya Magharibi “A” Unguja.
Dkt.Dimwa, amesema Zanzibar ni nchi ya visiwa vyenye ardhi ndogo yenye rutuba kubwa ambayo ikitumiwa vizuri kwa ajili ya kilimo cha kisasa itapunguza changamoto ya uingizaji wa chakula kingi kutoka nje ya Zanzibar.
Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, alisema wananchi wengi wanafanya kilimo cha mazoea hali inayosababisha kukosekana kwa ufanisi katika kilimo hicho kutokana na ukosefu wa utalaamu.
Aliitaka Wizara ya kilimo Zanzibar, kuongeza juhudi za kuwafikia wakulima katika maeneo mbalimbali nchini kutoa elimu ya kilimo cha kisasa na matumizi sahihi ya pembejeo ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 Zanzibar iwe na chakula cha kutosha.
Alieleza kuwa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ibara ya 145,imeweka mkazo juu ya sekta ya kilimo kuwa na nafasi maalum ya kuchangia mapinduzi ya kilimo kwa lengo la kujitoshereza kwa mahitaji ya chakula kuwa na ziada ya matumizi ya sekta nyingine ikiwemo za kiuchumi kama vile viwanda na huduma za biashara.
“Nakupongezeni kwa kazi nzuri ya kuendeleza maonesho haya ya kilimo ambayo ni fursa ya pekee kwa wakulima,wavuvi,wafanyabishara na wananchi mbalimbali wanaokuja hapa kujifunza na kupata elimu juu ya masuala mbalimbali yanayohusu kilimo,ufugaji,uvuvi,maliasili na sekta nyingine za kibiashara.
Wito wangu kwanza Wizara ya kilimo endeleeni kuwa wabunifu zaidi na kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto za kila mwaka ili kufanya vizuri na kwa utofauti kwa mwaka ujao kuhakikisha unaimarisha huduma na mahitaji ya wananchi wa makundi yote.”, alisisitiza Dkt.Dimwa.
Pamoja na hayo aliwasihi Wizara ya kilimo kuwekeza zaidi katika kufanya utafti mbalimbali wa magonjwa ya mazao,mifugo,mbegu za nafaka,mbegu za matunda na mboga mboga ili kupata ufumbuzi wa dawa za kutibu magonjwa hayo pamoja na upatikani wa mbegu bora zinazoendana na mazingira ya Zanzibar.
Alitoa wito kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kuweka utaratibu wa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya wavuvi kwa kuwakopesha zana za uvuvi zikiwemo boti za kisasa ili nao wajikwamue kiuchuma kama wanavyofanya kwa wakulima.
Dkt.Dimwa, alipotembelea Wizara ya Uchumi wa Bluu Zanzibar, aliwataka kuhakikisha wanatekeleza kwa ufanisi maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ili kufikia mwaka 2025 wawe wamekamilisha kazi hiyo.