NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Watumishi Housing Investment (WHI) kupitia Faida Fund imejipanga kuongeza juhudi za kuimarisha mfuko pamoja na kuongeza kasi ya kutoa huduma kwa wawekezaji pamoja na kushirikana na wadau wengine ili kutimiza malengo ya serikali.
Akizungumza leo Agosti 10, 2024 kwenye Mkutano wa mwaka wa wanahisa uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment (WHI) Dkt. Fred Msemwa, amesema kuwa wataendelea na juhudi za kuimarisha mfuko ili uweze kutumika katika kuandikisha wanachama wapya pamoja na kuthibitisha taarifa zao.
Dkt. Msemwa amesema kuwa lengo ni kuondoa changamoto katika mfumo wa mtandao, hivi karibuni litapata ufumbuzi.
“Mfumo huu umebuniwa na watanzania, hivyo hatujatumia fedha nyingi kuwalipa makampuni ya kigeni kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kutengeneza mfumo” amesema Dkt. Msemwa.
Amesema kuwa juhudi wanazofanya WHI zimesaidia kuchangamsha soko, huku akiwataka kuchangamkia fursa ya kujinufaisha kifamilia, vikundi pamoja na taasisi.
“Pia tuwafundishe watoto wetu namna ya kutumia fursa ya kuwekeza ili waweze kufanya vizuri wakati wakiwa wakubwa” amesema Dkt. Msemwa.
Mwanachama wa Mfuko wa Faida Fund Elizabeth Maico, amesema kuwa elimu ya uwekezaji inapaswa kutolewa kwa jamii ili kutambua fursa zilizopo.
Amesema kuwa wakati umefika wa kuchangamkia fursa ya kufanya uwekezaji kupitia Faida Fund jambo ambalo litawasaida kufanikisha shughuli za maendeleo hapo baadaye.
Nae Meshaki Robert, amesema kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo Nchi ni ukosefu wa elimu ya biashara ya fedha, hivyo nilianza kushiriki mafunzo ya elimu ya fedha ili kupata elimu hiyo.
Amesema kuwa Faida Fund ni mfuko wenye utaratibu rafiki wa kuchangia fedha wakati unawekeza kupitia Control namba tofauti na mifuko mengine ambapo fedha inaweza kupotea.