Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 10, 2024 jijini Dar es Salaam kuhusu Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi yanayotarajiwa kufanyika Agosti 19, 2024 hadi Agosti 30, 2024 Msasani Beach Club, Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Msemaji wa Jeshi Luteni Kanali Gaudentius Ilonda akizungumza na waandishi wa habari.
…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanatarajia kufanya mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi yatakayohusisha vikundi vya muziki wa dansi na ngoma za asili kutoka vikosi vya JWTZ yanayotarajiwa kufanyika Agosti 19, 2024 hadi Agosti 30, 2024 Msasani Beach Club jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuzinduliwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na kufungwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 10, 2024 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, amesema kuwa mashindano hayo ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ.
Meja Jenerali Mkeremy amesema kuwa mashindano hayo hayatakuwa na kiingilio hivyo wananchi wote wanakaribishwa kwenda kujionea burudani kutoka vikundi mbalimbali vya dansi pamoja na ngoma za asili.
“Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda ameaona ni vyema baada ya kuona sanaa na utamaduni vinapotea, hivyo akayaruhusu kuwe na ngoma za asili kwa mfumo wa mashindano” Meja Jenerali Mkeremy.
Meja Jenerali Mkeremy amesema kuwa mashindano haya yatakuwa endelevu ambayo yatafanyika kila mwaka, huku akieleza kwa mwaka huu 2024 kutakuwa na bendi 10 za muziki wa dansi na vikundi tisa vya ngoma za asili ambavyo vitashindanishwa.
Amesema kuwa mwaka huu vitashiriki vikundi vya JWTZ, hivyo kadri miaka inavyozidi kwenda wanaendelea kuboresha mashindano hayo kwa kuvishirikisha na vikundi vya kiraia na wasanii binafsi.
Meja Jenerali Mkeremy amesema katika kufanikisha mashindano hayo watashirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), huku akieleza kuwa na zawadi ambazo zitatolewa kwa washindi ni pamoja na kurekodiwa video na audio na nyimbo hizo zitapewa nafasi ya kutoa burudani kwenye Kilele miaka 60 ya JWTZ .