Na WAF – Ethiopia
Mawaziri wa Afya wa nchi za Afrika wanatarajiwa kukutana kwa dharura kabla ya mwisho wa mwezi Agosti kujadiliana, kupitisha mikakati pamoja na kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox) barani Afrika.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaalamu ya Mawaziri wa Umoja wa Afrika wanaosimamia Afya, Lishe, Idadi ya Watu na Udhibiti wa Dawa ametoa uamuzi huo Agosti 9, 2024 wakati wa kufunga kikao cha Tano cha kamati mahususi ya kitaalam ya Mawaziri wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) Jijini Addis Ababa, Ethiopia.
“Nimefikia uamuzi huu baada ya kikao hiki kupokea taarifa ya Taasisi ya African (CDC) kuhusu hali ya ugonjwa wa Mpox barani Afrika ambapo ilielezwa kuwa takribani nchi Tisa za Afrika zina wagonjwa na hivyo kuwepo hatari ya ugonjwa kusambaa katika nchi nyingine za Afrika.” Amesema Waziri Ummy
Amesema, taarifa ya African CDC ilionesha kuwa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Julai, 2024 jumla ya watu 14,250 wameathirika na ugonjwa huo wa Mpox na kati ya hao watu 456 wamefariki.
Aidha, wakati wa kuhitimisha kikao hicho cha Tano cha kamati mahususi ya kitaalam ya Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) wanaoshughulikia masuala ya Afya, lishe, Idadi ya watu na udhibiti dawa, Waziri Ummy amewapongeza washiriki wote wa kikao hicho.
Sambamba na pongezi hizo Waziri Ummy amewaelekeza nchi wanachama kutekeleza masuala yote yaliyokubaliwa katika Kikao hicho yakiwemo ya kufanya maboresho ya kisera kwa nchi wanachama sambamba na kutekeleza mipango ya Kitaifa ya kudhibiti magonjwa ya kuambikiza na yasiyo ya kuambukiza.
“Pia, tuendelee kuimarisha huduma za Lishe na Afya ya akili hususani kwa vijana na udhibiti wa bidhaa tiba zisizokidhi viwango na dawa bandia, nchi wanachama zimetakiwa kuandaa Mpango wa kupambana na bidhaa tiba duni na bandia ambao utajumuisha udhibiti wa bidhaa tiba mipakani.” Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesisitiza uimarishaji wa mtandao wa maabara za bidhaa tiba za nchi wanachama na kupunguza uagizaji wa bidhaa tiba kutoka nje ya Bara la Afrika na kuhamasisha uzalishaji wa ndani pamoja na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu athari za bidhaa tiba duni na bandia pamoja na kuandaa mfumo wa ukusanyaji wa bidhaa tiba duni na bandia.
Tanzania ndiye mwenyekiti wa kamati hii kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Agosti, 2024 hadi Agosti, 2026.