*Ataka Libebe Taswira ya Madini
Dodoma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa ameridhishwa na Maendeleo ya Ujenzi wa Mradi wa Jengo la Makao Makuu ya Wizara ya Madini unaoendelea katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma na kwamba, matarajio yake ni kuona mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) unakamilika kwa wakati.
Ameyasema hayo leo, Agosti 9, 2024 alipotembelea mradi huo ili kukagua maendeleo yake ambapo amempongeza Mkandarasi kwa juhudi anazoendelea kuzifanya ili kuhakikisha jengo hilo linakamilika kwa muda uliopangwa.
Aidha, Mhe. Mavunde amewataka Mkandarasi huyo pamoja na Mshauri Elekezi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kukamilisha jengo ndani ya muda uliopangwa ili Wizara iweze kutoa huduma kwa haraka na ufanisi kwa wadau kutokana na kupatikana kwa ofisi zote sehemu moja.
“Nawapongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Wizara kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko makubwa sana na mmezingatia ubora tulioutaka,’’amesema Mhe. Mavunde.
Pia, Waziri Mavunde amemhakikishia Mkandarasi na Mshauri elekezi kuwa Wizara itahakikisha inatimiza wajibu kwa upande wake ili kuhakikisha taratibu zote zinakamilika kwa haraka ili kuacha shughuli za kiufundi zikikamilika.
Katika hatua nyingine, Mavunde ameitaka Menejimenti ya Wizara na mkandarasi kuangalia namna ya ambayo itawezesha jengo hilo kubeba taswira ya Wizara ya Madini ambayo inakwenda sambamba na shughuli za Sekta ya Madini, na kuongeza “tunataka kuona utambulisho utakaoonyesha kuwa hapa ndiyo Wizara ya Madini,’’ amesisitiza Waziri Mavunde.
Naye, Mshauri Elekezi kutoka TBA Msanifu wa Majengo Weja Ng’olo amesema wana imani kubwa na Mkandarasi kukamilisha ujenzi huo kwa wakati kutokana na kuwasili kwa vifaa muhimu vitakavyowezesha kuendelea na hatua nyingine za ujenzi
Kwa upande wake, Mkandarasi kutoka (NHC), Mhandisi Peter Mwaisabula amesema Shirika litahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Ujenzi wa Jengo la Wizara lenye ghorofa tano (5) unagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 22. Hadi sasa ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 84.4.