Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) Mwalimu Gulam Abdallah (kushoto), akifuatiwa na
Makamu wa rais wa TOC Henry Tandau na Katibu Mkuu wa TOC, mkimbiaji Gabriel Gerald Geay, na Filbert Bayi (wa nne toka kushoto) akifuatiwa na Magdalena Crispin Shauri, Jackline Juma Sakilu, nahodha Alphonce Felix Simbu, mwalimu riadha Anthony Njiku Mwingereza na mwalimu wa Kuogelea Alexander Thomas Mwaipasi wakiwa wame relax pamoja katika kijiji cha Wanamichezo cha Paris 2024 katika kitongoji cha Saint Dennis baada ya wanariadha hao kufanya maoezi mepesi kujiandaa na kutupa karata za mwisho za Tanzania katika michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 inayohitimishwa wikiendi hii.
Pamoja na mambo mengine, mwalimu Abdallah, Tandau na Bayi wamekuwa wakikaa na wanariadha hao wakifanya nao mazungumzo ba kuwapa nasaha za kuwajenga kisaikolojia wakiwa tayari kushiriki mbio za Marathon, ambapo kesho Jumamosi Agosti 10 wataanza wanaume (Simbu na Geay) wakati Jumapili Agosti 11 itakuwa ni zamu ya wanawake, Sakilu na Shauri.
Ikumbukwe Bayi aling’aa katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 1974 huko Christchurch, New Zealand, alipovunja rekodi na kushinda medali ya dhahabu mbele ya aliyekuwa bingwa John Walker wa New Zealand na Mkenya Ben Jipcho kwenye mbio za mita 1500.
Katika ushindi huo, Bayi aliweka rekodi mpya ya dunia ya dakika 3:32.2, na Walker akaenda chini ya rekodi ya zamani ya dunia iliyowekwa na Mmarekani Jim Ryun.
Mchuano huo wa Bayi na Walker hadi leo unatajwa kama moja ya mbio kubwa zaidi za mita 1500 za wakati wote.
Baada ya Bayi kuweka rekodi hiyo ya mita 1500 mwaka 1974, mwaka mmoja baadaye (1975) katika Mashindano ya ‘Dream Mile’ huko Kingston Jamaica akavunja rekodi ya dunia ya mbio za maili moja iliyokuwa inashikliliwa na Mmarekani Jim Ryun.
Bayi pia alivunja rekodi ingine ya kuwa mmiliki kwa muda wa miaka 48 wa ile rekodi ya ubingwa wa mita 1500 ya Michezo ya Jumuiya ya Madola ambayo hatimaye ilikuja kuvunjwa mwaka 2022 kwenye michezo hiyo huko Birmingham, Uingereza.
Mwalimu Gulam Abdallah ni mchezaji na mwalimu wa michezo na kocha wa zamani wa Taifa Stars, wakati Tandau ni mtaalamu wa sports Medicine ambaye pia ni mhitimu wa shahada ya Olympic Masters.
Wakati huo huo, Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) imeamua kumaliza michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 kwa mbio za Marathon za wanawake, tofauti na miaka ya nyuma ambapo wanaume ndio waliokuwa wakimalizia.