Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali leo tarehe 9 Agosti, 2024 wameshiriki kwenye zoezi la upimaji wa afya kwa hiari lililofanyika katika Ofisi ya zamani ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora zilizoko Mtumba Jijini Dodoma.
Zoezi hilo la upimaji wa afya limelenga kuwahamasisha Watumishi wa Umma kujenga tabia ya kupima na kufahamu hali ya afya zao mara kwa mara, zoezi hilo limeratibiwa na kuandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Akizungumza baada ya kupata huduma ya upimaji afya, kwa niaba ya Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili wa Serikali Mkuu Bi. Catherine Paul amewapongeza wadau walioandaa zoezi la upimaji afya kwani utawasaidia Watumishi kufahamu hali zao za kiafya, “niwapongeze wahusika wote waliofanikisha zoezi hili, kwakuwa wametoa fursa kwa Watumishi kupima afya zetu, pia tumepata ushauri mzuri wa namna ya kuboresha na kutunza afya”.
Kwa upande wake Bi. Herieth Mpili akimuwakilisha Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Anuai za Jamii kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amefurahishwa na mwitikio mkubwa wa Watumishi katika ushiriki wa zoezi hilo, “mwitikio wa Watumishi kwenye zoezi hili umekuwa mkubwa, wamejitokeza kwa wingi na kupima afya huku baadhi yao wametaka zoezi hili liwe endelevu”.
Katika hatua nyingine Bi. Herieth amesema zoezi la upimaji wa afya kwa Watumishi wa Umma limelenga kuwahamasisha Watumishi wa Umma kupima afya zao, pia ni jitihada za Ofisi ya Rais Utumishi katika kuratibu na kusimamia udhibiti wa Magonjwa yasiyoambukiza mahala pa kazi.
Nae Afisa Msaidizi wa Afya wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Bi. Lilian Magawila amezungumzia baadhi ya Magonjwa yanayofanyiwa vipimo katika zoezi la upimaji wa afya kwa Watumishi wa Umma ni pamoja na, vipimo vya Moyo, Figo, Mac
ho, Mifupa, mfumo ya fahamu na koo, pamoja na mfumo wa mkojo na uzazi kwa akina baba na kina mama.