NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kuanza utekelezaji wa mradi wa Samia Housung Scheme wenye lengo la kujenga Nyumba 5,000, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga nyumba hizo katika maeneo ambayo bado hayafikiwa na mradi na yenye uhitaji.
Akizungumza na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) leo Agosti 9, 2024 Makao Makuu ya NHC Upanga, Dar es Salaam, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi, amesisitiza kutoacha malengo ya kuanzishaji kwa Shirika la Nyumba la Taifa lililoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere pamoja na kujenga nyumba zenye viwango vya hali ya juu ambazo zinaweza kununuliwa na wananchi wenye kipato cha chini.
Mhe. Ndejembi wakati umefika kwa NHC kuweka mipango ambayo itamsaidia mtu mwenye kipato cha chini kumiliki nyumba za NHC kupitia utaratibu rafiki.
“Mnapaswa kuanzisha utaratibu wa kulipa kiasi fulani cha asilimia ya gharama ya Nyumba na kuruhusu mteja huyo kuanza kuishi huku akiwa analipa kiasi kidogo cha fedha kila mwezi mpaka atakapomaliza deni lake” amesema.
Mhe. Ndejembi ametoa wito kwa menejimenti ya NHC kuhakikisha hakuna wizi wa vifaa vya ujenzi katika utekeleza miradi ya shirika la Nyumba jambo ambalo litasaidia thamani ya Nyumba kuendana na gharama halisi.