Na: Dk. Reubeni Lumbagala.
Tuliosoma somo la historia mada ya ukombozi wa nchi za Afrika (Nationalism and Decolonization of Africa), tumefundishwa na kusoma baadhi ya sababu mbalimbali zilizosababisha Waafrika kuchukua hatua ya kudai uhuru na ukombozi wa nchi zao, sababu mojawapo ni bei ndogo ya mazao ya Waafrika (Low prices of Africans crops). Wakoloni kama vile Waingereza, Wajerumani, Wafaransa, Wabelgiji, Waspania na wengine walijenga mazingira ya kuwafanya Waafrika kuwa maskini na watumwa wao kwa kuhakikisha mazao wanayolima yanauzwa kwa bei ndogo huku wakoloni hao wakiwa wanunuzi wa mazao hayo na kunufaika na mfumo huu wa kinyonyaji waliouweka.
Kutokana na dhamira ya wakoloni kutaka kuwanyonya Waafrika na raslimali zao, wakoloni walikuwa wakipanga bei ndogo ya mazao yaliyozalishwa na Waafrika ili kupata faida kubwa (super profit). Hali hii ikasababisha Afrika kuwa sehemu ya kuzalisha malighafi, huku malighafi hizo zikisafirishwa kwenda Ulaya na mabara mengine kutengeneza bidhaa na bidhaa hizo kuletwa Afrika na kuuzwa kwa bei kubwa.
Kutokana na bei ndogo za mazao na sababu nyingine, Waafrika wakaamua kupigana ili kujikomboa na kupata uhuru wao. Walifanya hivi ili kufurahia maisha ya uhuru yasiyo na unyonyaji. Waafrika walikuwa na kiu ya kutaka kuona bei nzuri ya mazao wanayoyazalisha kama vile kahawa, katani, pamba, chai, mahindi na mazao mengine. Walitaka bei ya mazao inayoakisi gharama za uendeshaji kwenye kilimo na hali ya maisha iliyopo kwa wakati husika.
Pamoja na mafanikio ya nchi za Afrika kupata uhuru, bado suala la bei nzuri ya mazao haijawa ya kuridhisha, bado mazao mengi ya wakulima wa Afrika na Tanzania ikiwemo yanauzwa kwa bei ndogo. Ili tutoke kwenye shida hii ya bei ndogo ya mazao ya wakulima, kunahitajika utashi mkubwa wa kisiasa wa viongozi wetu kuhakikisha wakulima wanafurahia jasho lao kwa kuhakikisha mazao ya wakulima yanawekewa bei elekezi ili kuinua hali za maisha ya wakulima wetu.
Kipekee, nimpongeze sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa hakika amekuwa mstari wa mbele kutetea na kulinda maslahi ya wakulima. Dhamira yake ya kuinua sekta ya kilimo haina chembe ya shaka kwani amekuwa akiongeza fedha kila mwaka kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo.
Ongezeko la raslimali fedha katika Wizara ya Kilimo kunatoa uhakika wa mabadiliko chanya ikiwemo suala la kuboresha hali za maisha ya wakulima kwa kuboresha kilimo nchini.
Kimsingi, kutokana na kazi ngumu ya kulima, kupalilia, kuhudumia na hatimaye kuvuna mazao, mkulima anayo haki ya kuuza mazao nzuri inayoendana na gharama za uendeshaji alizotumia wakati wa kulima hadi kufikia hatua ya kuvuna mazao yake. Bei nzuri ya mazao inaleta tabasamu kwa wakulima na kuwavuta wengi kushiriki kwenye kilimo na hivyo kuwa na usalama wa chakula nchini, kupata malighafi za uhakika, kukuza sekta ya viwanda na biashara, kuboresha hali za maisha za wakulima na kupata fedha za kigeni kwa kuuza mazao nje ya nchi.
BEI YA MAHINDI NA MPUNGA JUU
Rais Dk. Samia akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Rukwa pamoja na mambo mengine aliacha kicheko kwa wakulima kwa kutaka bei ya mahindi iongezeke. Mathalani, Rais Dk. Samia aliagiza Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua mahindi kwa bei ya shilingi 700 kwa kilo moja. “Waziri Bashe nakuagiza nendeni na bei ya shilingi 700 ya mahindi. Na msimu ujao twende na ruzuku ya mbegu za mahindi na mbolea” ameelekeza Rais Samia.
Bei nzuri ya mazao ni motisha kwa wakulima kuendelea kulima na kuwavutia wengine kushiriki kwenye kilimo. Bei nzuri inawafanya wakulima kuwa na mtaji wa kulima katika msimu mwingine, kuboresha maisha yao kwa kujenga nyumba za kudumu, kununua mahitaji muhimu ya watoto na wategemezi wao pamja na kufungua shughuli nyingine za kuwaingizia vipato kama vile maduka, vyombo vya usafiri na mengine mengi.
Vilevile, hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi Ifakara mkoani Morogoro, Rais Dk. Samia aliagiza bei ya mpunga iongezeke kutoka shilingi 570 hadi 900 kwa kilo moja. “Tumepokea kilio cha bei ya mpunga, hapa niseme kidogo, wakulima hawa wanapoteza nguvu kubwa. Naelekeza NFRA waje wanunue mpunga hapa tunatoka kwenye bei ya kilo 570 mnayolipwa hivi sasa na wengine tunakuja na bei ya shilingi 900” ameelekeza Rais Dk. Samia.
BEI NZURI YA MAZAO KUGUSA MAISHA YA WENGI
Ikumbukwe kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania kutokana na zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania kuwa ni wakulima. Kilimo pia ndiyo sekta yenye mnyororo mkubwa wa thamani kutokana na wengi kushiriki kwenye kilimo kwa namna tofauti tofauti. Mathalani, waliojiajiri na kuajiriwa kwenye kilimo watapata vipato vizuri kutokana na uwepo wa bei nzuri ya mazao. Ongezeko la wadau kushiriki kwenye kilimo kunatoa uhakika wa malighafi nyingi za viwandani, hali inayochochea ongezeko la viwanda na uzalishaji wake na kufanya wananchi wengi kupata ajira viwandani.
Aidha, wawekezaji wa sekta ya usafirishaji wa mazao kama vile mafuso na treni watakuwa na uhakika wa kufanya biashara zao kwa kusafirisha mazao, hivyo kuongeza mapato na vipato kupitia usafirishaji wa mazao. Sanjari na hilo, mafanikio ya kilimo yanachochea ukuaji wa sekta ya biashara kutokana na mazao yanayozalishwa kuuzwa katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Vilevile kilimo kinachangia maboresho na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji kama vile barabara, madaraja na reli. Zaidi sana, shughuli zote hizo zinaambatana na kulipa ushuru na kodi, hivyo basi, mapato ya ndani ya halmashauri zetu pamoja na serikali kuu zitakusanya fedha nyingi katika mnyororo wa thamani wa kilimo.
Nihitimishe kwa kusema kuwa, Rais Dk. Samia amethibitisha pasi na shaka kuwa yupo pamoja na wakulima katika kuwainua kiuchumi kama nilivyoeleza hapo juu,hivyo basi, ni wakati muafaka sasa serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi ili kuwavutia wananchi wengi kushiriki katika kilimo.
Katika kipindi hiki ambacho kuna tatizo kubwa la ajira kwa vijana na wahitimu wengi katika ngazi mbalimbali za elimu, kilimo, ufugaji na uvuvi ni sekta ambazo zinaweza kutusaidia sana kupunguza tatizo la ajira na kusaidia kukuza uchumi na maendeleo ya nchi yetu. Ufanisi wa sekta hizo pamoja na kufungua fursa za viwanda nchini, vijana wengi watapata ajira, uchumi utakuwa kwa kasi kubwa na nchi yetu kuwa na usalama wa chakula.
Dk. Reubeni Lumbagala ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.