Na Dk. Reubeni Lumbagala
Maendeleo na ukuaji wa uchumi unahitaji uwekaji wa mipango thabiti itakayofanikisha kutimia kwa azma ya maendeleo na ukuaji wa uchumi. Kwa kuwa serikali inawajibika moja kwa moja kwa mujibu wa katiba ya nchi kuboresha ustawi wa wananchi wake kimaendeleo, ndiyo maana mikakati mbalimbali inawekwa na serikali ili kufikia maendeleo na ustawi wa wananchi na nchi kwa ujumla.
Kimsingi, maendeleo katika sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara, viwanda, utalii na sekta nyingine unategemea sana uwezeshwaji kupitia sekta ya usafirishaji ambayo ni muhimu sana. Usafirishaji ni nyenzo inayoziwezesha sekta nyingine kupiga hatua kwani baada ya kumalizika shughuli za uzalishaji wa bidhaa au huduma hupaswa kusafirishwa kutoka eneo moja la uzalishaji kwenda eneo jingine. Usafirishaji kwa njia ya anga, majini na nchi kavu (barabara na reli) kwa pamoja ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi.
Moja ya njia ya usafiri ambao kama taifa tulikuwa hatuna tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu katika nchi yetu ya Tanzania ni reli ya kisasa ya mwendokasi (Standard Gauge Railway – SGR). Hayawi hayawi sasa yamekuwa, ilikuwa ni wazo la viongozi wetu ya kuwa Tanzania kwa hadhi yake inapaswa kuwa na reli ya kisasa ya mwendokasi ili iwezeshe kuwa nyenzo ya kukuza uchumi wa nchi.
Mchakato wa ujenzi wa SGR ulianza chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hayati Dk. John Pombe Magufuli. Uthubutu wake ulisababisha ujenzi kuanza mara moja na hata baada ya Mwenyezi Mungu kumchukua, mrithi wake ambaye ni Rais wa Awamu ya Sita Dk. Samia Suluhu Hassan aliendeleza ujenzi huo wa SGR kutoka Dar es Salaam – Morogoro –Dodoma, na sasa ujenzi umekamilika na wananchi wameanza kupata huduma ya usafiri huo.
MANUFAA YA SGR KIUCHUMI
Mosi, kupunguza muda wa safari. Muda ni mali, reli hii ya SGR ni ya mwendokasi inayopunguza saa za safari. Hivyo basi, watumiaji wake wataweza kuokoa saa za safari na hivyo kutumia saa chache na kuwahi katika shughuli zao mbalimbali za kiuchumi. Dunia ya sasa ya ushindani wa kiuchumi inafanya juhudi za kuokoa muda ili muda mfupi uweze kutumika kuzalisha tija kubwa kwa maendeleo. SGR ni mkombozi wa kuokoa muda na kurahisisha muda na hivyo kukuza uchumi kwa haraka. Kwa mfano, usafiri wa mabasi kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro takribani saa nne au zaidi lakini kwa reli ya SGR ni dakika 90 (saa moja na nusu).Usafiri wa SGR utasaidia usafirishaji wa haraka wa abiria na mizigo na hivyo kuongeza tija kiuchumi.
Pili, kuongeza makusanyo ya mapato ya serikali. Kupitia malipo ya nauli yanayofanywa na abiria au wasafiri wa reli hii, serikali inakusanya mapato. Kwa mfano, nauli ya daraja la kawaida Dar es Salaam-Morogoro ni sh. 31,000 huku Morogoro ikiwa sh. 13,000. Kwahiyo, malipo ya nauli ya abiria yanaiongezea serikali mapato kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC). Makusanyo ya mapato yanasaidia uwekezaji katika sekta nyingine kama kilimo, viwanda, uvuvi, biashara, uboreshaji wa huduma za kijamii kama elimu, afya, maji na umeme, na hivyo kusaidia nukuaji wa uchumi wa nchi.
Tatu, kuongeza fursa za ajira. Usafiri wa reli ya kisasa ya kisasa ya (SGR) umetoa fursa za ajira rasmi na zisizo rasmi. Ajira rasmi kama vile wafanyakazi walioajiriwa ndani ya TRC, makandarasi na watoa huduma mbalimbali na ajira zisizo rasmi kama vile wafanyabiashara katika stesheni za reli, waendesha bodaboda wamepata fursa za kujiongezea fedha kwa kufanyabiashara na kutoa huduma katika stesheni za Dar, Morogoro na Dodoma.
Nne, SGR itasaidia kudumu kwa barabara na kupunguza gharama za matengenezo ya barabara. Usafiri wa reli ni muhimu katika kusaidia barabara zidumu kwa muda mrefu, kwani baadhi ya mizigo mizito ambayo ilikuwa inasafirishwa kwa malori makubwa na kusababisha uharibifu wa barabara itaweza kusafirishwa kwa njia ya reli ambayo ni usafiri salama zaidi.
Pia, serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati wa barabara zilizokuwa zikiharibiwa na malori yenye kubeba mizigo mingi. Hivyo basi, SGR inakuwa mkombozi wa kutunza barabara na fedha nyingi zilizokuwa zikikarabati barabara zitatumika kuwekeza katika sekta nyingine za kimaendeleo na kijamii.
Kwahiyo, ujenzi wa SGR una manufaa lukuki ambayo kama taifa yatasaidia katika jitihada za kukuza uchumi wan chi yetu na kusaidia kuboresha hali za maisha ya wananchi.
TUTUNZE MIUNDOMBINU YA SGR
Nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kuwa wazalendo wa kutunza miundombinu ya reli hii ya kisasa. Fedha nyingi zimetumika na zinaendelea kutumika katika ujenzi wa reli hizi za kisasa katika mikoa mingine ya nchi yetu. Kila Mtanzania ana dhamana ya kuwa balozi wa kutunza na kulinda miundombinu ya reli hii badala ya kuwa mhujumu wa miundombinu. Ni jambo la fedheha kutumia kodi za wananchi kutengeneza reli halafu waibuke wananchi wachache waihujumu miundombinu kama vyuma na kuviuza ili kujipatia fedha. Haikubaliki Abadan asilani.
Kudumu kwa miundombinu ya reli ya kisasa kutaendeleza manufaa ambayo kama taifa tumeshaanza kunufaika nayo kupitia SGR. Pesa kidogo ambayo mtu anaweza kuipata kupitia uharibifu wa miundombinu ya reli isiwe sababu ya kuharibu faida kubwa ambayo nchi yetu inaipata. Wakazi wa vijiji na maeneo jirani kuzunguka SGR wanategemewa sana katika ulinzi wa miundombinu ya reli ya kisasa. Tunakila sababu ya kujivunia kufanikisha usafiri wa SGR na kuanza kula matunda yake.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.