NA JOHN BUKUKU, DODOMA
Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imejipanga kutumia Majukwaa mbalimbali kuwafikishia wananchi Elimu ya Bima ya Amana na Usalama wa Fedha.
Benki zote nchini vikiwemo vyombo vya Serikali vitafikiwa na elimu ya shughuli zinazofanywa na DIB na kuhakikisha wananchi wengi wanapata ufahamu kuhusu DIB inavyotekeleza majukumu ya kutoa kinga kwa wateja wenye amana katika benki pamoja kufilisi.
Akizungumza leo Agosti 7, 2024 katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB) Isack Kihwili, amesema kuwa lengo ni kuhakikisha watanzania wanapata elimu kuhusu DIB jambo ambalo litakuwa na tija.
Kihwili amesema kuwa lengo ni kutoa kinga kwa wananchi, wateja wenye amana katika mabenki pamoja kufilisi.
“Tumejipanga kutumia mitandao ya kijamii, vyombo vya habari pamoja na vyombo vya serikali ili wawe mabalozi wazuri na kuwafikia watu wengi” amesema Kihwili.
Kihwili amesema kuwa majukumu yao ni kulipa amana
mteja shilingi milioni saba na nusu baada ya benki kufilisika, hivyo kama mteja atakuwa anadai fedha zaidi atasubiri utaratibu wa ufilisi.
“DIB tutaendelea kufatilia madeni na fedha itakayopatikana tutawalipa baada ya madeni ya benki kulipwa” amesema Kihwili.
Akizungumzia maonesho ya nanenane amesema kuwa ni mara ya kwanza wanashiriki maonesho hayo wakiwa wamesimama wenyewe kwani miaka ya nyuma walikuwa wanafanya kazi chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kihwili amesema kuwa mwitikio ni mzuri katika maonesho kwani kuna idadi kubwa ya wananchi wamefika katika banda lao kwa ajili ya kupata elimu ambayo wameifurai kutokana ina umuhimu mkubwa kwao.
“Mawaziri, wabunge, viongozi mbalimbali wamehamasika kuja kutembelea banda letu pia wametupa ushauri kuhusu kuboresha maonesho yetu” amesema Kihwili..
Pia amewataka wateja ambao wanadaiwa na mabenki ambayo yamefilisiwa kutimiza uwajibu wao kwa kutoa ushirikiano wa kulipa madeni yao.
Akizungumzia bima za amana za fedha ambazo zipo katika mitandao ya simu, amesema kwa kushirikiana na taasisi zingine DIB waka katika mchakato wa kuandaa utaratibu utakaotumika kulinda fedha za wateja katika mitandao ya simu.
Bodi ya Bima ya Amana (DIB) ni Taasisi ya Serikali ambayo imeundwa kutoa kinga kwa amana kwa wateja wa benki na taasisi za fedha wakiwa na jukumu la kulipa fidia pale benki inapofilisika ukomo wa kinga hiyo ni shilingi milioni 7.5.