Benki Kuu ya Tanzania BoT imetoa rai kwa wakopeshaji nchini kuhakikisha nanatoa nakala ya masharti ya mkopo yenye lugha rahisi ambayo mkopaji atayaelewa na kujiridhisha kuchukua mkopo huo.
Wito huo umetolewa leo agosti 7,2024 jijini Dodoma kwenye maonesho ya Nanenane na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw. Emmanuel Tutuba wakati alipotembelea katika banda la Benki hiyo katika maonesho ya Nanenane jijini Dodoma.
Amesema Mkopaji anapaswa kujiridhisha na masharti ya mkopo,matumizi ya mkopo huo lakini uhimilivu wa kurejesha mkopo huo.
“Tunasisitiza mkopaji lazime asome masharti na ajiridhishe hayo masharti anaweza kuyamudu kwa sasa kwa maana kuna baadhi ya wakopeshaji wasio waadilifu wanaweka masharti kwa kificho kwa kiasi kikubwa ili mkopaji asiyafahamu”,Amesema Gavana Tutuba
Aidha Gavana Tutuba amewataka wakopaji wasichukue mkopo mkubwa kupita uwezo wao lakini pia fedha wanazokopa kuzielekeza kwenye shughuli za kiuchumi ili waweze kurejesha mkopo huo.
“Elimu ya fedha ni swala mtambuka na ni swala muhimu sana na hapa kwenye maonesho tunaendelea kutoa elimu ili kumuwezesha mtu kutafuta pesa kwenye njia halali aweze kuzitunza lakini awe na nidhamu ya pesa”,Amesema.
Amesema BoT wametoa miongozo kwa taasisi ndogo za fedha ambayo inamtaka mtu anapoenda kukopa fedha hata kama hana elimu ya fedha anapaswa azingatie viwango ambavyo ni himilivu kulingana na mazingira ya uchumi.
Sambamba na hayo amesema katika maonesho hayo wanatoa elimu ya namna mifumo ya fedha inavyofanyakazi lakini pia kuonesha namna uchumi ulivyokuwa imara .
“Tumeshiriki katika maonesho haya kuwaonesha wananchi namna uchumi wetu ulivyokuwa imara na unavyoendelea kusimamia vizuri taratibu zote za mabenki na mifumo ya kifedha”,Amesema.