Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu ametoa wito kwa Wananchi wa Kijiji cha Chitete, Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa kufanya maandalizi ya kuunganishiwa umeme (wiring) katika nyumba zao.
Ametoa wito huo hivi karibuni aliposhuhudia zoezi la kuwasha umeme katika kijiji hicho wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijijni Awamu ya Pili (R3R2) Mkoani Rukwa.
“Nimeshuhudia Umeme umefika hapa Chitete, ninawasihi kuchangamkia fursa hii adhim ya kuunganishiwa umeme kwa kuanza kufanya ‘wiring’ katika nyumba zenu,” amesisitiza Mhe. Balozi Kingu.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti Mhe. Balozi Kingu alipata wasaa wa kuzungumza na Wahandisi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Mkandarasi wa mradi huo wa R3R2 Mkoani Rukwa.
Aidha, Mhe. Mwenyekiti Kingu alimuelekeza Mkandarasi Kampuni ya Pomy and Quihaya JV awe amekamilisha kazi ya kuwasha umeme katika vijiji vyote ndani ya Mkoa huo ifikapo Agosti 31, 2024.