Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa akisajiriwa tayari kuanza kupata huduma ya Azampesa kwenye simu yake ya kiganjani kabla ya kuzindua Ushirikiano kati ya Kampuni ya Azampesa na Shirika la Posta Tanzania ngazi ya Kanda kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika katika uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya. Kulia ni Meneja wa Kanda wa Azampes, Victor Kihwili na Meneja wa wa Shirika la Posta Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Michael Mwanachuo. (Picha na Joachim Nyambo)
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua Ushirikiano kati ya Kampuni ya Azampesa na Shirika la Posta Tanzania katika ngazi ya Kanda kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika katika uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya. (Picha na Joachim Nyambo).
……….
Na Joachim Nyambo, Mbeya.
SHIRIKA la Posta Tanzania limepongezwa kwa ubunifu wa kujiunga na Kampuni ya Azampesa katika utoaji wa huduma za kifedha hatua inayotajwa kuwa ya kimapinduzi itakayolifanya Shirika hilo kuendelea kuhimili ushindani wa soko.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa alitoa pongezi hizo jana alipozindua Ushirikiano kati ya Kampuni ya Azampesa na Shirika la Posta Tanzania ngazi ya Kanda kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika katika uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.
Malisa alisema kutokana na ujio wa teknolojia ya mawasiliano wadau wengi walipata mashaka juu ya maisha ya Shirika la Posta kwakuwa huduma nyingi ilizokuwa ikizifanya zimekuwa na mabadiliko makubwa ikiwemo utumaji wa barua.
Alisema lakini ubunifu unaoendelea kufanywa na uongozi wa shirika hilo unaonesha kuwa limejizatiti kuhakikisha linamudu ushindani wa kibiashara uliopo jambo alilosema ni la msingi na ni muhimu ubunifu zaidi wa kuja na bidhaa tofauti tofauti za kihuduma ukaendelea.
“Tunaamini wananchi wengi watafikiwa na huduma hii na lengo la kuongeza mjumuisho wa wananchi kwenye mnyororo wa fedha litakuwa limefikiwa.”
“Ni vitu vipya tunaanza kuviona kwenye Shirika letu la Posta..tulikuwa tunahofu pengine ushindani umekuwa mkubwa lakini ubunifu huu ni mzuri na tunaamini sasa watarudi sokoni na watarejea kama tulivyokuwa tukiwajua tulipokuwa tukiwaona wenyewe.” Alisema Malisa
Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza ujio wa ushirikiano wa Azampesa na Shirika la Posta kuwezesha wananchi wakiwemo wakulima kuachana na kutembea na fedha nyingi mikononi hatua inayohatarisha usalama wao bali sasa watumie njia ya mitandao kufanya malipo au kusafirisha fedha.
Aliwakaribisha wawekezaji wengine wanaotaka kuja na bunifu zao watumie fursa mbalimbali zilizopo mkoani Mbeya na Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini ikiwepo kwenye sekta za kilimo ili kuwezesha wananchi kuwa na nafasi nzuri zaidi ya upatikanaji wa huduma.
Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Posta Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Michael Mwanachuo alisema ushirikiano baina ya pende hizo mbili unayo maana kubwa kwakuwa utawezesha kufikisha huduma alipo mwananchi hasa kutokana na Shirika hilo kuenea katika maeneo mengi nchini.
“Shirika la Posta lina mtandao mkubwa sana, tuna ofisi takribani wilaya zote nchini hivyo kwa ushirikiano huu tutaweza kutoa huduma mijini na kuzifikisha vijijini.” Alisema.
Naye Meneja wa Azampesa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Victor Kihwili alisema ushirikiano huo umekuja katika wakati muafaka kwakuwa pamoja na kusaidia utoaji wa huduma za kifedha pia unaongeza upatikanaji wa ajira hususani kwa vijana.