Na Neema Mtuka
RUKWA
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Daniel Chongoro ameipongeza Halmashauri ya Kalambo mkoani Rukwa kwa kuanzisha teknolojia mpya ya ukaushaji wa dagaa na samaki kwa kutumia kaushio la kisasa (solar tent drier) ambalo litawezesha upatikanaji wa samaki na dagaa wenye ubora na kuwezesha wavuvi kujikwamua na hali ya kiuchumi.
Ameyasema hayo baada ya kutembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kupitia maonesho ya wakulima nanenane yanayofanyika kikanda Jijini Mbeya na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya Kalambo kwa kuanzisha teknolojia hiyo ambayo itawezesha kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvuliwa hususani kipindi cha masika.
Awali akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda ,Afisa uvuvi wilayani humo Bw. Abdul Balozi ,Amesema sambamba na teknolojia hiyo pia wameleta bidhaa mpya ya unga wa samaki ambayo ni ya kwanza kwa kanda ya nyanda za juu kusini ambayo itasaidia kupunguza udumavu na utapiamlo kwa watoto kutokana na unga huo kuwa na virutubisho vyote muhimu.
‘’Unga huu utaweza kutumiwa na watu wote ikiwemo watoto wachanga,na watu wazima na katika kuhakikisha huduma hii inapatika sehemu zote za mwambao wa ziwa Tanganyika kwa kushirikina na mradi wa FISH4ACP tumejenga makaushio makubwa matatu na jiko moja la kubanikia samaki katika vijiji vya Kasanga, Kilewani na Samazi’’,alisema Bw. Balozi.
Kwa upande wake mkuu wa Divisheni ya kilimo , mifugo na uvuvi Bw. Nicholas Mrango amesema licha ya hilo Halmshauri imetenga fedha milion sitini na moja ( 61,000,000/=) kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe ikiwemo kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya vyakula bora kwa lengo la kutokomeza tatizo la udumavu wilayani humo.
Kushoto ni mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhe.Daniel Chongolo akimsikiliza Afisa Wanyamapori msaidizi wilayani kalambo Bi. Aneth Umbella baada ya kutembelea banda la Halmashauri ya Kalambo kupitia maonesho ya wakulima Nanenane jijini Mbeya.www.kalambodc.go.tz