Umoja wa Afrika (AU), umeviomba vyombo vya habari barani Afrika kuandika vizuri habari za Afrika ikiwepo masuala ya uhamaji wafanyakazi ndani ya Afrika na nje ya Afrika.
Kumekuwepo na ongezeko la uhamaji wa wafanyakazi kutoka watu 17.2 millioni mwaka 2010 hadi kufikia watu 26.3 millioni mwaka 2019.
Uhamaji huo wa wafanyakazi umeingiza mapato ya fedha za kigeni katika nchi za Afrika kutoka dola billion 55 mwaka 2010 hadi kufikia dola billion 86.4 mwaka 2019 hata hivyo kumekuwepo na upotoshwaji wa jambo hili hasa na vyombo vya habari vya nje.
Akizungumza katika warsha ya siku tatu ya kuwajengea uwezo viongozi wa wafanyakazi katika vyama vya waandishi wa habari Afrika, Wahariri na Waandishi waandamizi inayoendelea *mjini* Dakar nchini Senegal, Mkuu wa Kitengo cha Kazi, Ajira na Uhamaji katika Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dk *Sabelo* Mbokazi alisema vyombo vya habari vya Afrika vina wajibu *kuiandika vizuri na kueneza ujumbe halisi kuhusu umuhimu wa uhamaji katika maendeleo ya nchi za Afrika* .
Alisema kwa sasa kutokana na ukuaji wa teknolojia Duniani kumekuwepo na ongezeko la habari za uongo na upotoshwaji kuhusu bara la Afrika.
“Nyie kama viongozi wa wanahabari Afrika mnawajibu kusaidia kuandika mambo yenye manufaa kwa Afrika”alisema
Dk Mbokazi, pia alitoa wito kwa Waandishi wa Habari kuchukua jukumu kubwa katika kuhakikisha Kunakuwepo na mazingira bora ya Uhamiaji wa kazi barani Afrika.
Hata hivyo alisema AU itaendelea kulinda na kuheshimu Uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza barani Afrika.
Rais wa Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ) Omar Faruk Osman alisema watendaji wa vyombo vya habari wanapaswa kutumia wingi wa vyanzo vyao ili kufichua ukiukaji wa kazi na kuboresha utawala wa Uhamaji wa Wafanyakazi barani Afrika.
Osman alisema, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wanahabari wanapaswa pia kuhamasisha waafrika kufanya kazi zenye staha nje ya nchi zao,kulipwa vizuri lakini kulindwa kwa haki zao.
Akitoa Takwimu juu ya uhamiaji wafanyakazi ndani ya Afrika na nje ya Afrika, *Afisa wa takwimu, katika kitengo* Cha uhamaji wafanyakazi wa Umoja wa Afrika, Brian Okengo alisema kumekuwepo na ongezeko la uhamiaji wafanyakazi katika utafiti ambao umefanywa kuanzia mwaka 2010 hadi 2019.
Okengo alisema licha ya ongezeko la watu Kila mwaka pia kumekuwepo na ongezeko la fedha za kigeni kutokana na Takwimu _zilizokusanywa barani Afrika._
“Kumekuwepo na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni Kila mwaka na kwa Takwimu ya AU kuanzia mwaka 2010 hadi 2019 mapato yameongezeka kutoka dola billion 55.5 *hadi* kufikia dola billion 86.4″alisema
Alisema miongoni mwa sababu ambazo zimekuwa zikichangia ongezeko la watu kuhama katika mataifa yao ya asili ni masuala ya kiuchumi,kisiasa,masuala mazingira katika nchi zao,masuala ya kijamii *na teknolojia* .
Awali akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Serikali ya Senegal, Ousseynou Dieng kwa niaba ya Waziri wa wa Mawasiliano, alitaka waandishi barani Afrika kuungana kuandika vizuri bara la Afrika.
Dieng alisema bara la Afrika bado haliandikwi vizuri katika masuala mbalimbali ya maendeleo na kueleza serikali ya Senegal itaendelea kushirikiana na wanahabari kufanya kazi zao vizuri kwa manufaa ya wananchi.
Kamisheni ya AU ya Kazi, Ajira na uhamaji kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) na Shirikisho Waandishi wa Habari Afrika (FAJ) wamezindua mpango wa pamoja kuhusu Uhamiaji wa Wafanyikazi barani Afrika.
Warsha hiyo Inaendelea katika hoteli ya Dakar’s Ndiambour ikilenga kujenga uwezo wanahabari kuhusu masuala ya Uhamiaji wa Wafanyakazi barani Afrika Tanzania katika warsha hiyo inawakilishwa na Chama cha Wafanyakazi Katika Vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA).