Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda vifaa vya michezo mipira ya miguu katika hafla fupi iliyofanyika leo Agusti 5, 2024,Dar es Salaam.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda akizungumza na waandishi wa habari leo Agusti 5, 2024, Dar es Salaam wakati wa akipokea mipira 500 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika hafla fupi iliyofanyika leo Agusti 5, 2024, Dar es Salaam.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limepokea vifaa vya michezo mipira ya miguu 500 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kufanikisha shughuli mbalimbali za michezo katika jeshi na kufanikiwa kupiga hatua.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agusti 5, 2024, Dar es Salaam wakati wa akipokea mipira 500 kutoka TFF, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda, amesema kuwa jeshi linashiriki michezo mengi, hivyo vifaa hivyo vitasaidia kuendelea kufanya vizuri.
Jenerali Mkunda amesema kuwa michezo sehemu ya kazi, hivyo wataendelea kuongeza bidii hasa mchezo wa beach soccer ambao umeonekana kuwa na fursa kubwa ya kufanya vizuri, huku akieleza kuwa wameuchukua na wanakwenda kuufanyia kazi kwa kina na kufanya uwekezaji uenda baadaye wakawashangaza watu.
“Tunaona Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyokuwa pamoja katika masuala ya michezo, hivyo ni bahati sana kuona kiongozi wa juu kushiriki michezo kwa kiwango hicho, haswa katika kutia hamasa kwa timu zetu zinaposhiriki michuano ya kimataifa” amesema Jenerali Mkunda.
Amesema kuwa wametambua TFF imegundua kuwa jeshi ni wadau wakubwa wa michezo na kwa sasa wana vituo vya michezo ambazo mipira hiyo itapelekwa kwa ajili ya kwenda kufanyia mazoezi.
Jenerali Mkunda amemshukuru Rais wa TFF Wallace Karia kwa kutoa vifaa vya michezo kwa JWTZ, huku akitoa wito kuendelea kusaidia timu za jeshi ili wafanye vizuri.
Rais wa TFF Wallace Karia amesema kuwa wataendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kuwapa vifaa vya michezo vitakavyo kwenda kutumika kwenye vituo vya michezo vya jeshi hapa nchini ili kuwekeza kwenye mpira wa miguu.
“Hii ni ahadi ambayo TFF tuliitoa na leo tumetimiza kwa kutoa mipira 500 pamoja na yote naomba nitumie nafasi hii kuwaomba mtusaidie kuboresha viwanja ikiwemo soka ikiwemo cha Uwanja wa Lake Tanganyika uliopo Kigoma ambao unatumiwa na timu yenu ya Mashujaa” amesema Karia.