Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Fakii Raphael Lulandala (katikati) akizungumza kwenye kikao na wajumbe wa eneo tengefu la Mirerani juu ya changamoto zinazowakabili wachimbaji ndani ya ukuta anaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite
………………
Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Fakii Raphael Lulandala, ametoa siku saba kwa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira jiji la Arusha (AUWSA) kufikisha maji kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani.
Lulandala akizungumza baada ya kumalizika kikao cha eneo tengefu la Mirerani, amesema ametoa siku saba kwa AUWSA ili wachimbaji wa madini ya Tanzanite waweze kupata maji.
“Tumetoa maelekezo kwa AUWSA ndani ya siku saba kuhakikisha maji yanapatikana ndani ya migodi na maeneo yote yanayozunguka ukuta wa madini ya Tanzanite,’ amesema Lulandala.
Amesema baada ya kupita siku hizo saba na maji kupatikana AUWSA waanze mchakato wa kutandaza miundombinu ya kufunga mabomba ya maji uanze kwenye machimbo hayo.
“Baada ya hapo mpango wa kupeleka maji kwenye machimbo ukifanyika kuna maelelekezo tutayatoa kwani kuna maeneo ambayo wenye migodi wanapaswa kupata maji,” amesema DC Lulandala.
Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa AUWSA, Justin Rujomba amesema wamejipanga kutekeleza agizo hilo la mkuu wa wilaya kwa kufikisha huduma ya maji kwa wachimbaji madini.
Rujomba amesema watafanikisha hayo kupitia mipango miwili ambapo mpango wa muda mfupi watatekeleza kwa kutumia magari kisha mpango mrefu watasambaza maji ya bomba.
Amesema gari hilo litakuwa linabeba maji na kuingiza ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite na kuweka kwenye matenki.
“Kwenye mpango wa muda mrefu tunatarajia kutumia Sh8.3 bilioni na itakuwa suluhisho ya kupatikana kwa maji safi na salama kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite,” amesema Rujomba.
Amesema kwenye mpango wa muda mfupi wataingiza maji kupitia magari yatakayokuwa yamebeba maboza ya lita elfu 10 wakitumia bei elekezi ya serikali ambayo imepangwa na (EWURA).
“Magari yatakuwa yanachota maji safi na salama yaliyopo mji mdogo wa Mirerani na kuyaingiza ndani ya ukuta unaozunguka madini ya Tanzanite kwa kuyamwaga kwenye matenki yaliyopo ndani,” amesema.
Amesema baada ya hapo watatimiza mpango wa muda mrefu wa kufikisha maji kwani wameshafanya utafiti na kusubiria fedha hizo Sh8.3 bilioni ambazo zitafanikisha miundombinu ya maji.
Mmoja kati ya wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite, Bahati Mushi amesema hatua ya upatikanaji maji kwenye eneo hilo itakuwa maendeleo makubwa kwani maji ni uhai.
“Wachimbaji tukipata maji itakuwa vyema mno na tunampongeza Waziri wa Maji Jumaa Aweso ambaye anafanya kazi kubwa kuhakikisha watu wa maeneo mbalimbali wanapata maji,” amesema Mushi.