Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu (Sera,Bunge na uratibu) Ummy Nderiananga amewapongeza mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Dodoma(DUWASA) kwa utendaji wao huku akiwataka kuendelea kuchapa kazi katika kuwahudumia wananchi ili kutimiza lengo la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan la kumtua mama ndoo kichwani.
Pongezi hizo amezitoa leo Agosti 4,2024 kwenye maonesho ya Wakulima nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
“Endeleeni kufanyakazi kwa bidii ili mtimize lengo la Rais la kumtua mama ndoo kichwani hongereni sana kwa huduma mnayoitoa katika makao makuu ya nchi”,Amesema.
Kwa upande wake Muhudumu Wateja Leila Jumanne akimuwakilisha mkurugenzi mtendaji DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema katika kutatua changamoto za maji jijini hapo wameendelea kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo wa Nzuguni wa kisima kirefu chenye mita 300.
Amesema mradi huo utaenda kutatua changamoto ya maji katika jiji hilo ambapo mpaka kufikia mwezi disemba mradi huo utakuwa umekamikika.
“Tunaamini mpaka kufikia mwezi disemba hatutakuwa na changamoto ya maji katika mji huu mipango mbalimbali inaendelea ili kufiki hapo”,Amesema.
Akizungumzia mita za maji za kabla ya matumizi amesema tayari kunabaadhi ya maeneo tayari zimefungwa na wananchi wanaendelea kuzitumia.