Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imeridhishwa na huduma za udhibiti zinazotolewa na TASAC na kuifanya bandari ya Dar es salaam na bandari kavu kutekeleza Kanuni ya Ulinzi na Usalama wa mizigo bandarini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Jason Rweikiza (MB) leo tarehe 02 Augosti, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa LATRA jijini Dar es salaam amesema wamefurahishwa na TASAC katika kusimamia utekelezaji wa kanuni kwa wadau wake.
“Sisi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo tumefurahi na kuona udhibiti unaotolewa na TASAC katika kusimamia kanuni hiyo unatekelezwa na wadau vizuri.” Amesema Mhe. Rweikiza.
Aidha, Kamati imeweza kupokea maoni ya wadau wanaodhibitiwa na TASAC na kueleza kuwa wanashirikiana vizuri na TASAC pindi wanapowasilisha changamoto katika kutoa huduma bandarini TASAC hufanyia kazi kwa uharaka.
“Tunafanya kazi vizuri na TASAC na inapotokea changamoto yeyote TASAC hukaa pamoja na sisi kutusikiliza na kuitatua kwa haraka” Amesema Bw. Mathew Clift, Afisa Mkuu wa Fedha wa DP World.
Aidha, Bw. Clift ameongeza kuwa, DP World kwa muda wa miezi minne tangu waanze kutoa huduma bandarini wameweza kuhudumia Meli kwa wakati na kuweza kupunguza muda wa Meli kusubiri kuingia gatini kutoka siku 30 hadi siku 7 tu. Hii imepelekea kupunguza gharama kwa mlaji wa mwisho na kuongeza shehena na mapato ya nchi.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile amesema kuwa kamati hiyo ndio hupitia kanuni zinazosaidia utendaji kazi za udhibiti na kupelekea utoaji wa huduma bora na salama katika bandari zetu.
“Leo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imefanya ziara ofisi za TASAC, Bandari kavu na hatimae bandari ya Dar es Salaam. Katika ofisi za TASAC wamepitishwa kwenye wasilisho la Kanuni ya Ulinzi na Usalama wa Mizigo katika maeneo ya Bandari na Bandari kavu”, amesema Mhe. David Kihenzile (MB) na Naibu Waziri wa Uchukuzi.
Kamati hiyo imefanya ziara ya kutembelea ofisi za TASAC zilizopo jengo la SUMATRA, Bandari kavu za PMM 2001 “Limited”, GALCO, TRH na ghati namba 8 hadi 11 ya meli za makasha zinazohudumiwa na Tanzania East Africa Getway Terminal Limited (TEAGL), gati namba 0 hadi 7 inayoendeshwa na DP World.
TASAC ni Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania iliyoanzishwa mwaka 2018 chini ya Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania Sura 415 ikiwa na majukumu ya kudhibiti Usalama, Ulinzi wa Vyombo vya Usafiri Majini na Utunzaji wa mazingira Majini, Udhibiti wa Huduma ya Usafiri Majini na Kufanya Biashara ya Huduma za Meli katika bidhaa mahsusi.