Muogeleaji chipukizi Sophia Anisa Latiff leo Jumamosi Agosti 3, 2024 ameingia bwawani na kutupa karata ya tatu ya Tanzania kwenye michuano ya Paris 2024, akishika nafasi ya nane katika heat yake iliyokuwa na jumla ya washindani wa idadi hio hio, akitumia sekunde 28:42
Mshindi wa kwanza Jovano Kuljaca kutoka Montenegro alitumia sekunde 27:19 ikiwa ni sawa na sekunde 1:23 tu zaidi ya Sophia.
Kwenye mchuano huo wa kuogelea wa mita 50 Freestyle kwa wanawake kulikuwa na jumla ya washindani 79 ambapo kwa nafasi yake Sophia amekuwa mtu wa 49 kiujumla, akiwa kawapita wenzie 30.
Sophia, ambaye ni muogeleaji mchanga na mwenye tumaini kubwa ya kuiwakilisha Tanzania kwa muda mrefu siku za usoni, leo amefunga rasmi pazia la awamu ya kwanza ya ushiriki wa Tanzania katika michezo ya Olympiki ya Paris 2024 iliyokuwa na wachezaji watatu – yeye, muogeleaji mwenzie Collins Phillip Saliboko na mcheza Judo Andrew Thomas Mlugu.
Karata nne za mwisho za Tanzania zitatupwa na wakimbiaji Marathon, ambao watawasili Agosti 7, wakitokea kambini Arusha moja kwa moja, tayari kwa mbio hizo zitazokuwa Agosti 10 na Agosti 11, 2024.
Safari hii mfumo wa michuano ya Marathon umebadilishwa, ambapo tofauti na ilivyozoeleka, wanaumendio wataanza kukimbia na wanawake ndiyo watamalizia.
Hivyo basi, wakimbiaji wa Marathon kwa wanaume, yaani nahodha Alphonce Felix Simbu – nahodha na Gabrield Gerald Geay watashindana mnamo Agosti 10, 2024
Wakimbiaji wa Tanzania wa Marathon kwa wanawake, Jackline Juma Sakilu na Magdalena Crispin Shauri wamepangwa kukimbia Agosti 11, 2024, ambayo ndiyo siku ya mwisho ya Michezi ya Olimpiki ya Paris 2024.