Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mussa Zungu amewataka wahititimu wa chuo Cha Ufundi stadi Furahika kufanya kazi kwa bidii na kujiendeleza kitaaluma zaidi kwani elimu haina mwisho
Zungu ameyasema hayo katika mahafali ya 19 ya chuo hicho yaliyofanyika katika viwanja vya chuo,Buguruni Malapa Jijini Dar Es Salaam.
“Niwapongeze kwa kuhitimu mafunzo yenu katika kada mbalimbali,Jambo ambalo ni muhimu zaidi na msiishie hapo mlipoishia na badala yake mjiendeleze zaidi kitaaluma katika ushindani wa soko la ajira”amesema.
Aidha Zungu amesema ajira zipo za kutosha endapo wahitimu watajituma na Kuwa wabunifu zaidi katika kukuza taaluma zao kwa kupitia ubunifu kwani unahitajika Sana katika ulimwengu wa sasa.
“Serikali imeweka mazingira wezeshi ambayo kipaumbele chake ni vijana,hivyo ni wajibu wenu kujituma na kufanya kazi kwa bidii popote mtakapoajiriwa au kujiajiri”amesema.
Amewaasa wahitimu hao Kuwa na nidhamu huko waendako kwani watakuwa mabalozi wazuri wa Chuo hicho.
Hata hivyo Naibu Spika pia ameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuunga mkono jitihada za Rais Dkt Samia katika suala la elimu kwa kutoa elimu ya Ufundi kwa vijana tena bila malipo na kuahidi kusaidia baadhi ya changamoto zinazokikabili Chuo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chuo Cha Furahika,Dkt David Msuya ameiomba serikali kuchangia vifaa vya kuendeshea Chuo hicho kwani wanatoa elimu bila malipo huku mwanafunzi akichangia Shilingi elfu hamsini pekee kwa ajili ya mitihani.
“tukushukuru Sana Naibu spika na nikuombe utuchangie kompyuta pamoja na viongozi wenzako ikiwemo vyerehani na vifaa vingine kwa ajili ya kufundishia kwa vitendo hivyo kwa msaada huo mtakuwa mmewasaidia wanafunzi wa Chuo chetu”amesema
Dkt Msuya amesema jumla ya wahitimu 45 wamehitimu mafunzo ya stadi za kazi (Ufundi)katika fani mbalimbali na wengi waliohitimu katika Chuo hicho wameajiriwa katika sekta mbalimbali hapa nchini.
Ameongeza Kuwa wameamua kutoa elimu ya Ufundi kwa vijana wa kike na kiume ili kusaidia kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya na biashara ya kuuza miili kwa vijana wa watoto wa kike ambayo husababishwa na vijana hao kukosa elimu ambayo huwasaidia kupata ajira au kujiajiri.