Wananchi wa wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu kwa kuhakikisha wanazingatia usafi katika mazingira yao yanayowazunguka
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa mkutano wake wa hadhara na wananchi wa kata ya Kirumba katika viwanja vya Kabuhoro gengeni kwaajili ya kusikiliza kero na changamoto ambapo amewasisitiza kufanya usafi na kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya dhidi ya kujikinga na ugonjwa huo
‘.. Ugonjwa wa kipindupindu hauchagui, Na ule ni ulaji wa kinyesi kibichi, Sasa wewe uchafu upo mbele yako na hautaki kuutoa ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula amemtaka mtendaji wa kata hiyo kuwachukulia hatua watu wote wanaochafua mazingira kwa makusudi kwa sababu watachangia kuenea kwa ugonjwa huo
Wesa Juma Nabahani ni diwani wa kata ya Kirumba ambapo mbali na kumpongeza Mbunge huyo kwa mchango wake katika kusukuma maendeleo ameishukuru Serikali kwa kupanga kutekeleza mradi wa Maji taka ndani ya kata yake kwa kuwa utasaidia utunzaji wa mazingira pamoja na kuepusha ueneaji wa magonjwa ya tumbo na kuharisha
Nae mtendaji wa kata ya Kirumba Gaudencia Venance Msilikali amefafanua kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha kata hiyo inakuwa safi ikiwa ni pamoja na kuendesha kampeni ya usafi na mazingira inayopambwa na kauli mbiu ya “Mtaro wangu, Nyumba yangu” sanjari na usimamizi wa sheria za usafi na mazingira
Faida Juma na Imelda Daud ni wananchi wa mitaa ya Kabuhoro na Ibanda Ziwani kata ya Kirumba ambao licha ya kuipongeza Serikali na kuishukuru kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo wamelalamikia zoezi la upimaji shirikishi na miundombinu mibovu ya barabara za mitaa zilizoharibiwa na mvua hivyo kuomba ukarabati wa barabara hizo
Mbunge wa Jimbo la Ilemela anaendelea na ziara Jimboni kwake akiambatana na wataalam wa manispaa ya Ilemela na wakuu wa taasisi zote zinazopatikana ndani ya Jimbo hilo