Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi · MHE. Daniel Baran Sillo (Mb), amesema Serikali kupitia wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itahakikisha inakamilisha ujenzi wa vituo vya Polisi 77 Nchi nzima vilivyoanzishwa kujengewa kwa nguvu za wananchi.
Mhe. Sillo ametoa kauli hiyo Agosti 02, 2024 akiwa Mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi ambapo amekagua ujenzi wa jengo la Zahanati ya Polisi lililojengwa kwaajili ya Idara ya Kinywa na Meno, ujenzi wa Nyumba za kuishi Askari kisha kukagua Ujenzi wa kituo cha Polisi Nyegezi uliofikia hatua ya uezekaji kilichojengwa kwa nguvu za wananchi.
Akiwa katika ziara hiyo, Mhe Sillo amesema Serikali kupitia wizara ya mambo ya ndani ya nchi itahakikisha inakamilisha ujenzi wa vituo hivyo 77 vya Polisi kikiwemo kituo hicho cha Nyegezi katika mwaka wa fedha 2024-2025.
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Sillo ameongeza kuwa Serikali kupitia wizara hiyo itajenga vituo vingine vya Polisi 12 kwenye kata mbalimbali pamoja na kuboresha makazi ya Nyumba za kuishi Askari wa Jeshi la Polisi kwa kutumia fedha za mfuko wa tuzo na tozo.