Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Holle Makungu akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha miezi mitatu.
………
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imebaini dosari mbalimbali katika Miradi mitatu kati ya Miradi 10 iliyo fanyiwa uchunguzi yenye thamani ya ya zaidi ya shilingi milioni 28 ndani ya miezi mitatu pamoja na kubaini mianya ya Rushwa katika mifumo 7 ya uchambuzi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa TAKUKURU wa MkoaTemeke Bw. Holle Makungu wakati akizungunza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaamu juu ya tathimini ya utendaji katika kipindi cha miezi mitatu ambapo amesema licha ya kubaini dosari na mianya hiyo wametoa ushauri wa kufanyiwa kazi ili kuepusha upotevu wa mapato katika miradi ya maendeleo.
Amesema katika hatua nyingine wamebaini ukiukaji wa sheria ya ujenzi kwa kampuni ya sahara limited kwa kujenga jengo la vyumba sitini eneo la hifadhi ya barabara eneo la Mbagala ambapo wameamuru kuvunjwa kwa jengo hilo agizo ambalo limedaiwa kupuuzwa hali iliyo walazimu kuchukua hatua za kuwafikisha Mahakamani wamiliki wa jengo hilo.
Taasisi hiyo imesema inaendelea kutoa elimu kwa Umma Ili kutokomeza Rushwa huku wakiwaomba Wananchi kuendelea kushirikiana nao kwa kutoa taarifa za viashiria vya Rushwa ili kuitokomeza.