Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman akizungumza na wananchi wa Kisiwa cha Kojani Wilaya ya Wete Pemba mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Skuli ya Msingi ya Kojani inayojengwa ya Ghorofa (G+2) na Mkandarasi Kampuni ya Scenic Construction & Consultance Ltd ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kukagua miradi ya maendeleo inayojengwa Kisiwani Pemba.
……….
Na Masanja Mabula Pemba
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali itaendelea kujenga skuli kubwa na za kisasa zitakazokidhi mahitaji yote ya wanafunzi kuanzi ngazi ya msingi hadi Sekondari ili kuwaondolea changamoto wanafunzi ya kuingia mikondo miwili jambo ambalo linarejesha nyuma maendeleo ya elimu nchini.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Skuli ya Msingi Kojani Makamu wa Pili wa Rais amesema dhamira ya Rais Dkt Mwinyi ni kuhakikisha kila mtoto wa kizanzibari anapata haki yake ya msingi ya kusoma katika mazingira mazuri yatakayozalisha wataalamu wa fani mbali mbali watakaolisaidia Taifa katika harakati za maendeleo.
Aidha Mhe.Hemed amesema Serikali imejipanga katika kuwaletea maendeleo endelevu wanachi wake hivyo hakuna eneo leolote ndani ya Zanzibar litakaloachwa nyuma kimaendeleo ikiwemo visiwa vidogo vidogo vilivyopo Unguja na Pemba.
Sambamba na hayo Makamu wa pili wa Rais amesema suala la ujenzi wa Daraja, hospitali na vyooo katika kisiwa cha Kojani Serikali itakaa na kuangalia uwezekano wa kufanya ujenzi huo awamu kwa awamu kwa kuangalia kipaombele cha uhitaji wa wananchi wa kisiwa hicho.
Pia Amewataka wananchi wa Kojani kuzidisha umoja na ushirikiano katika suala zima la maendeleo sambamba na kuilinda na kuidumisha amani iliyopo nchi kwani ndio msingi wa maendeleo katika nchi yoyote ile duniani.
Nae Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Abdulghulam Hussein amesema mipango ya Wizara ya elimu ni kuhakikisha wanajenga skuli mpya na za kisasa, kuzifanyia ukarabati mkubwa skuli zilizoanza kuchakaa na kuongeza idadi ya madarasa iili kuondoa changamoto ya msongamano wa wanafunzi madarasani katika kisiwa cha Kojani na visiwa vyengine vilivyoopo Zanzibar.
Amesema kuwa wizara itaendelea kusimamia maslahi ya walimu pamoja na kuajiri walimu wapya kila skuli ili kuongeza ufanisi wa ufanyaji wa kazi utakaopelekea kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu na kupata wataaalamu ambao wataisaidia jamii na Taifa kwa ujumla.
Nao wananchi wa kisiwa cha kojani wameishukuru serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwawekea miundombinu mizuri ya elimu kwa watoto wao jambo ambalo litawasaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi sambamba na kuahidi kuwa skuli hio wataitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa faida ya vizazi na vizazi.