Ushirikiano baina ya viongozi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo umetajwa kuwa chachu kubwa inayosaidia kuharakisha ukamilishwaji wa miradi mingi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Nyanguku, Halmashauri ya Mji wa Geita, Elias Ngole, wakati wa sherehe ya kuwapongeza wenyeviti wa mitaa na vijiji wanaomaliza muda wao na kujipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
“Wenyeviti wangu wa mitaa ni viongozi muhimu sana. Tunatamani wasiwe kama makarai yakitumika yanatupwa. Hawa ni watu wenye mchango mkubwa sana. Kutokana na namna walivyonisaidia katika utekelezaji wa miradi ya serikali, tumeshirikiana nao kila siku. Nimeona ni muhimu kutambua mchango wao kwa kukutana nao na kuwapongeza kwa kuwapa hati za pongezi kwa kazi nzuri walizofanya kusaidia usimamizi wa miradi ya maendeleo katika Kata yetu,” alisema Elias Ngole.
Aidha, Diwani Ngole alisema hakuna sababu ya viongozi kuendelea kurumbana na kushindana katika kuwahudumia wananchi. Ni vyema kila mmoja akatambua nafasi yake bila kuingiliana majukumu, siri ambayo imemsaidia kufanya vizuri na kuwa na ushirikiano mkubwa na wenyeviti wake wa serikali za mitaa.
“Sisi viongozi tunatakiwa kujitathmini tulipotoka. Madaraka tunayapata kutoka kwa wananchi, hatutakiwi kubeba sifa nyingi na kuwasahau wananchi wetu. Niseme tu, tutaendelea kuwatambua na kuwapongeza wenyeviti wote ambao wamefanya vizuri katika Kata yetu ya Nyanguku. Hatutaishia leo tu,” alisema Elias Ngole.
Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa mitaa, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakato, Charles Kulola, alimshukuru Diwani kwa jinsi alivyoisaidia kufikia malengo ya kuwahudumia wananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali.