Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dkt. Bill Kiwia akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 1, 2024 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji wa Mikopo , Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dkt. Peter Mmaa akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 1, 2024 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu, Habari na Mawasiliano Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Omega Ngole akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 1, 2024 jijini Dar es Salaam.
Afisa Mawasiliano Mwandamizi Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Eline Maronga akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 1, 2024 jijini Dar es Salaam.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) katika mwaka wa masomo 2024/2025 imetenga shilingi bilioni 787 kwa ajili ya wanafunzi wanufaika 245,000, huku wakiwakumbusha waombaji wa mikopo kufata taratibu za uombaji ikiwemo kusoma kwa umakini miongozo ili kuepuka kujaza taarifa ambazo sio sahihi katika mfumo pamoja na kuzingatia muda wa uliotolewa wa kuomba mkopo kuanzia Juni 1, 2024 hadi Agosti 31, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 1, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dkt. Bill Kiwia, amesema kuwa wamefanya tathmini na kubaini baadhi ya waombaji wa mkopo kutosoma miongozo iliyotolewa ambayo ipo katika tovuti ya bodi : www.heslb.go.tz na kusababisha kukosea.
Dkt. Kiwia amesema kuwa miongozo inaelekeza waombaji wanapaswa kuhakiki vyeti vya kuzaliwa au vya vifo vya wazazi RITA au Wakala wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA) lakini baadhi hawafanyi hivyo na kushindwa kuendelea na maombi.
“Tunawashauri wazazi na walezi kuwawezesha watoto wao kwa ajili ya kufanya maombi ya mkopo badala ya kuwaombea kwani uzoefu unaonesha mwanafunzi akiomba mwenyewe maombi yanakuwa kamilifu” amesema Dkt. Kiwia.
Dkt. Kiwia amesema kwa sasa ni wakati wa kufanya maboresho kwa wanafunzi wahitaji wa mikopo ambao wamekosea kujaza taarifa muhimu kabla ya dirisha la maombi kufungwa Agosti 31, 2024.
Amesema kuwa pia wanafunzi wenye sifa za kuomba mkopo kupitia ‘Samia Scholarship’ wanapaswa kusoma taarifa katika tovuti ya bodi kwani maombi yanatarajia kuanza Agosti 3, 2024.
Dkt. Kiwia amesema kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha wanafunzi wanapata mkopo kwani jumla ya wanufaika wa mwaka wa masomo unaomalizika wa 2023/2024 walikuwa 224, 056 wakiwewo wanafunzi 78, 979 wa mwaka wa kwanza na kufanya ongezeko la jumla ya wanufaika 20,944.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mine, bajeti ya mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka bilioni 570 kwa mwaka 2021/2022 na kufikia bilioni 787 kwa mwaka 2024/2025.
“Kuongezeka kwa bajeti kumesababisha ongezeko la idadi ya wanufaika kutoka 177, 615 mwaka 2021/2022 hadi kufikia 250,000 mwaka wa masomo 2024/2025” amesema Dkt. Kiwia.
Katika hatua nyengine Dkt. Kiwia amewakumbusha wahitimu wa shahada ya TEHAMA kufanya maombi kushiriki mafunzo kwa ajili ya kuongeza ujuzi pamoja na kupanua wigo wa kuajiriwa.
“Julai 23, 2024 tulitoa tangazo kupitia tovuti yetu : www.heslb.go.tz kuhusu fursa za mafunzo ambayo yanatolewa bure, napenda kuwakumbusha zimebaki siku nne kufikia tarehe ya mwisho ya kupokea maombi kupitia mtandao wa Adanian (https://dlt.adanianlabs.io) ambapo mwisho wa kujaza fomu Agosti 5, 2024” amesema Dkt. Kiwia.
Makundi ambayo yanatarajia kupata mikopo na ruzuku ni pamoja wanafunzi wa shahada za awali (Undergraduate Degrees), wanafunzi wa stashahada (Diploma), stashahada ya juu ya mafunzo ya uanasheria (Post Graduate Diploma in Legal Practice), shahada za uzamili na uzamivu (Master and Phd Student) pamoja na wenye ufaulu wa juu katika tahasusi za sayansi katika mitihani inayoendeshwa na Baraza la Mithiani la Taifa (NECTA) ambao wanastahili kuomba ‘SAMIA Scholarships’