Meneja wa mizani TANROADS makao makuu,Injinia Leonard Mombia akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha.
………..
Happy Lazaro,Arusha .
Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) wameanza kufunga kamera kwenye mizani ili kuunganisha kwenye mfumo wa serikali kwenye vituo vya mizani nchi nzima kwa lengo la kudhibiti udanganyifu kwa magari yanayozidisha mzigo na kukwepa faini.
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Meneja wa mizani TANROADS makao makuu,Injinia Leonard Mombia wakati akizungumza katika mkutano wa tisa wa kimataifa wa wabunifu miundombinu na usafirishaji endelevu Afrika (ICTA) unaofanyika siku mbili jijini Arusha na kuwahusisha wakandarasi kutoka ndani na nje ya nchi.
Mombia amesema kuwa ,tayari hadi sasa hivi jumla ya vituo 13 zimeshafungwa kamera ambapo mkakati uliopo ni kufunga kwenye vituo vyote nchi nzima .
“Vituo vya mizani 13 ambazo zimeshafungwa kamera hizo na kuunganishwa kwenye mfumo wa serikali ni pamoja Mikese,Mikumi,Mpemba,Songwe, Makuyuni.,Njuki,Singida,Nara, Kimokoa,na Vigwaza mkoani Pwani.”amesema Mombia.
Aidha ameongeza kuwa,TANROADS imeamua kuondoa malalamiko ya muda mrefu yanayosababisha msongamano wakati wa kupima uzito kwenye mizani ya kawaida kwa kufunga mizani inayopima gari ikiwa inatembea (WEIGH IN MOTION (WIM)katika vituo mbalimbali vya mizani.
“Baadhi ya maeneo ambayo tayari mizani hizo zishamefungwa ni pamoja na Namanga, Vigwaza,Mikese,Mikumi,Wenda, Mpemba,Nara,Rubana na Njuki na imeonyesha .”amesema Mombia.
Amefafanua kuwa, hadi sasa TANROADS imefanikiwa kufunga mizani 80 katika mikoa tofauti kwa ajili ya kupima magari yanayozidisha uzito ili kudhibiti uharibifu wa barabara zilizotengezwa na serikali kwa gharama kubwa.
Hata hivyo amesema idadi kubwa ya madereva wamekuwa na uelewa mkubwa kuhusu matumizi ya barabara kutokana na faini pamoja na elimu inayotolewa na TANROADS.
Ambapo amesema kiwango cha faini na uzidishwaji wa mizigo umepungua ambapo kwa mwaka uliopita uzidishwaji wa mzigo ulikuwa asilimia 0.26 ikilinganishwa na mwaka 2020 faini zilikuwa kubwa na kufikia zaidi ya asilimia 20 .
Hata hivyo Meneja alitoa ushauri kwa wasafirishaji wazingatie vigezo na msharti yaliyopo katika ubebeji wa mizigo .